DAR ES SALAAM, TANZANIA
MKWAJU wa penalti uliopigwa dakika ya nne na Kipre Tchetche, ulitosha kuiwezesha Azam FC kushinda bao 1-0 dhidi ya Oljoro JKT, Jumatano na kuipiga kumbo Simba katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara..
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi Complex – nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Azam ilipewa penalti na refa Livingstone Lwiza kutoka Kagera baada ya mchezaji Yasin Juma wa Oljoro kushika mpira katika eneo la hatari.
Dakika ya 88, Himid Mao wa Azam alilimwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Amir Omari wa Oljoro.
Kwa matokeo hayo, Azam imefikisha pointi 24 baada ya kushuka dimbani mara 12 na kuishusha Simba yenye pointi 23. Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 26.
Katika mechi nyingine iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, mabingwa wa mwaka 1988, Coastal Union walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Morogoro wanaoburuza mkia.
Daniel Lyanga ndiye aliyekata mzizi wa fitina kwa bao la dakika ya 15, lililotosha kuiweka Coastal nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 22.

No comments:
Post a Comment