Pages

Thursday, March 21, 2013

Shule ina darasa moja, mwalimu mmoja wilayani Bagamoyo, Pwani

SHULE ya Msingi Machala iliyopo Kata ya Miono, wilayani Bagamoyo, Pwani, inakabiliwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa, hali inayosababisha wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba kusomea katika chumba kimoja.

Pamoja na tatizo hilo, shule hiyo yenye wanafunzi 155, inahudumiwa na mwalimu mmoja tangu ilipoanzishwa miaka saba iliyopita.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Christopher Lutuku, anatumia chumba cha stoo kama ofisi yake ya kuhifadhia vitabu na nyaraka mbalimbali za kiofisi.
Hayo yalibainika juzi mjini Miono katika kikao cha Halmashauri Kuu ya kata hiyo kilichoandaliwa na Mbunge wa Chalinze, Said Bwanamdogo, kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wakazi wa kata hiyo pamoja na kuelezea yale aliyoyafanya katika kipindi cha miaka miwili na nusu tangu achaguliwe.

Akitoa changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mihuga, Omari Nguya, alisema shule hiyo tangu ianzishwe miaka saba iliyopita inahudumiwa na mwalimu mmoja na kuongeza kuwa mwalimu mwingine aliyepangiwa katika shule hiyo hivi karibuni hayupo.
Kutokana na hali hiyo, alimuomba mbunge huyo kuharakisha kushughulikia tatizo hilo ili waweze kuletewa walimu wengine na kupata fedha za ujenzi wa madarasa.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lutuku alisema kwa mara ya kwanza mwaka huu shule hiyo inatarajia kutoa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba, lakini matumaini ya kufaulisha ni madogo, kwani baadhi ya vitabu vya darasa la saba hakuna na hata madarasa mengine wanatumia kitabu kimoja kimoja kwa baadhi ya masomo na vya masomo mengine hakuna kibisa.

Bwanamdogo aliahidi kushughulikia suala hilo haraka kuanzia ngazi ya Ofisa Elimu wa Wilaya, ili shule hiyo iweze kupata walimu, vitabu na fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na ofisi ya mwalimu.

No comments:

Post a Comment