Pages

Sunday, July 1, 2012

Fiesta 2012 Ni Bhass


*Tamasha lile lile, muonekano tofauti
* Kumwaga magari sita, Pikipiki 14, Simu 200, na zagazaga kibao!
Mtiti wa kuelekea tamasha kubwa na zuri la burudani la kila mwaka linaloratibiwa na Clouds Media group, maarufu kwa jina la Fiesta unatarajiwa kutimka kuanzia Jumapili ijayo katika viwanja vya TIA jijini Mbeya ambapo Bonanza la mashabiki wa timu za Ulaya watamenyana katika kinyang'anyiro cha Fiesta Soccer Bonanza, ikiwa ni sehemu tu ya shamrashamra ya tamasha hilo kwa mwaka huu.

Michezo hii itaendelea kwa mikoa kadhaa ikiwa ni sehemu tu ya shamra shamra hizo lakini pia kutakuwa na matamasha madogo madogo kama kumsaka MC Shujaa, kusaka kundi bora la kucheza muziki, shindano ambalo limepachikwa jina la Dance la Fiesta, na Fiesta Supa Nyota ambayo itamtoa mwimbaji mkali kabisa ambaye hajawahi kuonekana kwenye tasnia hii ambayo yatafuatiwa na ziara ya mikoa 14, kusherehekea mwaka mwingine wa mafanikio ya kiburudani kwa amani huku mashabiki wa muziki wa kizazi kipya wakiburudika na kujumuika kwa pamoja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kussaga ameiambia Mwananchi Starehe kwamba hili ni Tamasha la 11 tangu kuanzishwa kwake, na ni tamasha ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta hamasa kwa mashabiki wa muziki ambao kwa siku za nyuma ilikuwa ngumu kwao kukutana uso kwa uso na msanii wanayempenda.

"Fiesta ndiyo mwanzilishi wa mkutano wa uhakika wa uso kwa uso kati ya shabiki na msanii ambapo hapo awali ilikuwa ni mpaka msanii aalikwe, au afikirie mwenyewe kwenda lakini Fiesta ni uhakika wa msanii anayevuma kukutana na shabiki wake kwa wakati muafaka".

Kussaga aliitamka rasmi kauli mbiu ya tamasha hilo mwaka huu kuwa burudani itakuwa ile ile lakini muonekano ndio utakuwa tofauti kwani jukwaa litakuwa sio lile ambalo watu wamelizoea na pia kutakuwa na vyombo vya muziki ambavyo vitamsababishia shabiki wa muziki kupata muziki mzuri masikioni mwake usiokuwa na bugudha, ambao pia ataufurahia.

Tamasha la mwaka huu pia linatarajia kuwazawadia mashabiki wake magari sita yenye thamani ya shilingi milioni nane kila moja, aina ya Toyota Vitz, Pikipiki aina ya Boda boda takriban kumi na nne huku kila moja ikiwa na thamani ya shilingi Milioni moja na nusu, Simu 200, huku hamsini kati ya hizo ziliwa ni Blackberry zenye thamani ya shilingi laki saba kila moja na zilizobaki zikiwa ni Nokia dabo dabo zenye thamani ya Tshs 80,000.

Kuhusu wasanii watakaoshiriki kwenye tamasha hili, Kussaga ameiambia Starehe kwamba kutakuwa na wasanii wachanga ambao hawajawahi kuonekana katika jukwaa, na pia kutakuwa na wasanii wakubwa kabisa ambao kwa pamoja wataunganisha nguvu na kuleta kitu kikubwa na kizuri kwenye tasnia ya burudani ambacho mwisho wa siku kila mmoja wa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya atafurahia.

Shughuli nzito inaanza Julai, ambapo shughuli mbali mbali zitakuwa zikifanywa kwa kwezi mzima na baada ya hapo sasa mwezi wa nane ndio kitu kizima cha Fiesta yenyewe kitaanza.

Shughuli ya dace la Fiesta itafanyika katika mikoa ya Arusha Jumamosi hii, katika Club ya Mawingu, na kisha wiki zinazofuata itahamia kwenye mikoa ya Mwanza katika Club ya lips tarehe 7 Julai, kisha La Cassa Chica Tanga tarehe 14 Julai na kisha Maisha Club, Dar es Salaam, itakuwa ni Julai 17.

Mpaka sasa, shughuli ya Soccer Bonanza imeidhinishwa kwa mikoa minne tu ambayo ni Mbeya, mwanza Moshi na dar es Salaam.
Kuhusiana na Mc Shujaa, mpaka sasa ni dar, mwanza na Arusha ndio kunaonekana kwenye ratiba, lakini kadri muda unavyozidi kuendelea uongozi umeahidi kutoa ratiba endelevu.

Mikoa ambayo Fiesta itapita kwa mwaka huu imeidhinishwa kuwa ni Moshi, Arusha, Musoma, Shinyanga, Mwanza, Morogoro, Dodoma, iringa, Mbeya Singida, Tabora, Tanga, Zanzibar, na kisha Dar es salaam

No comments:

Post a Comment