TAASISI ya Mashekhe na Wanazuoni wa Kiislamu nchini, imeunga mkono kauli
ya hivi karibuni ya Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba
ya kuwataka Waislamu na Watanzania kote nchini kushiriki kikamilifu
katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26 mwaka huu.
Akizungumza
jana kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jopo la Mashekhe na Wanazuoni wa
Kiislamu nchini, mmoja wa mashekhe hao, Shekhe Hamis Mattaka alisema
wamelazimika kufanya hivyo kutokana na kuwepo kwa baadhi ya makundi
yanayowapotosha waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi juu ya ushiriki
wao katika sensa.
Alisema wao kama jopo
la wanazuoni, hawaoni tatizo la zoezi hilo kutokana na umuhimu wake kwa
taifa na kuongeza kuwa Sensa ya Watu na Makazi ipo kwa mujibu wa sheria
za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jopo
hilo limeiomba Serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa takwimu
zinazohusu dini za Watanzania zinazotolewa na vyanzo mbalimbali ndani na
nje ya nchi kwa kuwa kipengele hicho si sehemu ya sensa nchini.
“Tunajua
kuwa Serikali ilikuwa na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika
sensa hapana budi nia njema hiyo ya Serikali ilindwe kwa kuweka sheria
itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za Watanzania” amesema Shekhe
Mattaka.
Alifafanua kuwa, sensa ya
awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa na baadaye
kuondolewa katika sensa zilizofuata kwenye madodoso ya kukusanyia
takwimu za kaya.
“Sisi kama jopo kila
siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi hii ni wajibu wetu
kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya kutii sheria bila shuruti, kwa
hiyo tunasema Sensa ya Watu na Makazi ni jambo la kisheria si jambo la
mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo ambalo liko wazi kisheria
na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi wenyewe.”
Aliongeza
kuwa, Sensa ya Watu na Makazi itaiwezesha Serikali kupanga mipango ya
maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali ya kipato
cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha Serikali kuwapatia huduma
bora wananchi wake.
Katika hatua
nyingine jopo la mashekhe na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imewataka
wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya
Katiba mpya.
via HabariLeo
No comments:
Post a Comment