Pages

Monday, July 2, 2012

UDOM yakanusha madai ya kuwepo ufisadi chuoni hapo

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), umekanusha kuwepo kwa ufisadi chuoni hapo unaodaiwa kufanywa na chuo hicho kwa kushirikiana na benki moja mjini Dodoma katika kutafuna ada za wanafunzi.

Katika taarifa ya ufafanuzi ya chuo hicho iliyotiwa saini na Ofisa Uhusiano wa UDOM, Beatrice Baltazary, ilieleza kuwa habari hiyo iliyoandikwa na gazeti hili toleo lililopita, ilikuwa na upotoshaji.
Miongoni mwa ufafanuzi huo ni kwamba wanafunzi wote wanatakiwa kulipa gharama zote zinazoambatana na kupata elimu chuoni hapo mara wanapoanza mwaka wa masomo.
Kwa mujibu wa ufafanuzi huo, utaratibu uliotolewa na mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa kulipiwa ada na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, unamlazimu mwanafunzi kusaini ili kuthibitisha fedha kupokelewa chuoni na wale wasiosaini fedha hurejeshwa bodi na deni hubakia kwa mwanafunzi.

“Wanafunzi wengi wamekuwa wakikaidi kuthibitisha kupokea fedha za ada nia yao ikiwa ni kutaka kusoma bila kulipa ada na kwa kufanya hivyo wanakuwa hawana deni katika bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, hivyo basi chuo kimechukua hatua ya kuzuia vyeti vyao hadi watakapo maliza…” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ufafanuzi huo umekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuandika malalamiko ya wanafunzi wanaolipiwa ada zao na Bodi ya Mikopo kudai kuwa ada zao hutafunwa na chuo hicho kwa kushirikiana na benki moja uya mjini Dodoma.

Wanafunzi hao walidai kuwa licha ya kulipiwa ada na bodi, na wao kulipia kiasi cha asilimia walizopangiwa, lakini uongozi wa UDOM umekuwa ukiwalazimisha kulipa tena ada kwa maelezo kuwa hakuna rekodi zinazoonyesha kuwa walilipiwa ada na bodi.
Hata hivyo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Philipo Mulugo, aliahidi kufuatilia suala la bodi ya mikopo na kulitolea ufafanuzi.
 Via Gazeti la Nipashe

No comments:

Post a Comment