WANASHERIA wametoa maoni tofauti kuhusu mgogoro wa madaktari unaoendelea nchini na Serikali inavyoushughulikia, baadhi wakidai Serikali ipo sahihi, wengine wakipinga kwa madai kuwa imeingilia mahakama.
Wakili wa Kujitegemea, Harold Sungusia alisema kuwa kitendo cha Rais kutoa maelekezo kwa madakatari siyo tatizo, lakini maelezo yenye uamuzi ni kuingilia uhuru wa mahakama. Julai mosi katika hotuba yake kwa taifa, Rais Jakaya Kikwete pamoja na mambo mengine alizungumzia mgogoro wa madaktari akielekeza kuwa daktari anayetaka kufanya kazi arudi kazini na asiyetaka ajiondoe mwenyewe. Akizungumzia kauli hiyo ya Rais, Sungusia alisema:
"Kitendo hicho ni kuingilia uhuru wa mahakama, wakati ambapo bado Mahakama Kuu haijatoa uamuzi wake kuhusu kesi iliyofunguliwa Mahakama ya Kazi na Serikali dhidi ya madaktari." Alisema kuwa kuna mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu ya taifa aliyoitaja kuwa ni Dola, Mahakama na Bunge akieleza kuwa kwa kauli hiyo ya Rais Kikwete, Serikali imetumia vibaya dhana ya uhuru wa mahakama ambayo ni moja ya misingi ya utawala bora.
Alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kukosoa watu wanaojadili jambo lolote lililo mahakamani, wakati huohuo yenyewe imekuwa ikiingilia katika utendaji wake. “Serikali ni ya kwanza kukosoa watu wanapojadili jambo fulani kwa kisingizio kuwa lipo mahakamani. Wakati huohuo yenyewe ndiyo ya kwanza kuingialia mahakama,’’ alisema Sungusia. Wakili huyo alisisitiza kuwa Serikali imekuwa ikiingialia uhuru wa mahakama kila mara, akitolea mfano kesi ya mgombea binafsi .
Alieleza kuwa wakati kesi ya mgombea binafsi inaendelea mahakamani, Serikali iliamua kurudi bungeni haraka na kubadilisha kipengelea ndani ya Katiba kuzuia mgombea binafsi kuwania nafasi ya uongozi. Naye Mwanasheria Pendael Munisi alisema Bunge linaweza kujadili jambo hilo kwa kuwa linahusisha masilahi ya umma kwa mujibu wa Ibara 63(3)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.
‘’Ibara hiyo inaeleza kuwa Bunge linaweza kutekeza mamlaka yake na wabunge wanaweza kumuuliza waziri yeyote, jambo lolote kama linahusu masilahi ya umma,’’alisema Munisi.
Mwanasheria huyo alilisitiza kuwa Ibara 4 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, inaelezea mgawanyo wa madaraka kwa mihimili yote mitatu ambapo kila mhimili utatekeleza kazi zake kwa mujibu wa katiba na haipaswi kuingiliana katika uamuzi yake. Hata hivyo, alisema kuwa upande mwingine mgawanyo huo wa madaraka kivitendo haupo, kwa sababu Rais anaweza kuamua jambo lolote kwa masilahi ya umma na kwamba hatua hiyo ya Rais Kikwete ni kulinda uhai wa wananchi ambao maisha yao yapo hatarini kwa mgomo huo wa madaktari.
Alisema kuwa ili mihimili hiyo mitatu ifanye kazi bila kuingiliana kiutendaji sheria zote zinapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa na kuondoa mkanganyiko ulipo huku akitolea mfano wa kifungu cha 64 (1)© kinachomkataza mbunge kujadili jambo lililo mahakamani wakati Ibara ya 100 na ile 63(3)(a) inaeleza uhuru wa Bunge kujadili jambo kwa masilahi ya umma.
Naye Wakili wa Serikali Tumaini Kweka alisema haoni kama Serikali imeingilia uhuru wa mahakama akiwataka wananchi kujisomea na kujua sheria badala ya kukurupuka.
Mwanasheria Mwandamizi Francis Kayichire alisema Serikali ipo sahihi kwa kuwa, mahakama ikishatoa hukumu Serikali inatekeleza majukumu yake.
Alisema mahakama ilishaeleza kuwa mgomo wa madaktari ni batili hivyo Serikali inapaswa kuchukua hatua kwa wale wanaokwenda kinyume na mahakama.
Imeandaliwa na Aisha Ngoma, Daniel Mwingira na Pamela Chilongola na Geofrey Nyang’oro e&p
VIA: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment