Pages

Monday, November 26, 2012

Mgogoro wa Sekondari Bagamoyo, serikali kuchukua hatua.

Serikali imeamua kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya wanafunzi na walimu katika shule ya Sekondari Bagamoyo mkoa wa Pwani kufuatia mgogoro uliotokea na kusababisha shule hiyo kufungwa Novemba 5, mwaka huu.
Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Mafunzo ya Ufundi, Eustella Bhalalusesa akisoma ripoti ya uchunguzi jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya waziri, Dk Shukuru Kawambwa alisema wanafunzi waliothibitika kuwa vinara wa vurugu bila kutaja idadi yake watachukuliwa hatua za kinidamu ambazo hakuzieleza.
Pia alisema walimu walioonekana kutowajibika ipasavyo nao watachukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.

Alisema shule hiyo ilifungwa siku hiyo baada ya kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa amani na utulivu kitendo ambacho wizara yake iliamua kuunda kamati kuchunguza chanzo cha mgogoro.
Dk Kawambwa alisema uchunguzi umebaini kuwa, chanzo kikuu cha mgogoro huo ni mfarakano kati ya uongozi wa shule na baadhi ya wanafunzi ambapo kulitokea kutoelewana na mabadiliko ya kinidhamu yaliyotangazwa shuleni hapo.
Pia alisema mkuu huyo wa shule aliwataka wanafunzi watie mkazo katika masomo yao kitendo ambacho baadhi ya wanafunzi walikipinga na kusababisha kuwepo kwa mgogoro huo.

Alisema kamati hiyo imegundua kuwa kukosekana kwa umoja wa kikazi miongoni mwa walimu, utoro wa walimu kazini na utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi kumechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa mgogoro huo.
Alisema serikali imeamua, ili kutoa nafasi kwa uongozi wa shule kujipanga upya, wanafunzi wote waliothibitika kutoshiriki katika mgomo watarudi shuleni mwezi Januari mwakani kwa utaratibu utakaowekwa.

Alisema kwa wanafunzi wa kidato cha sita ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwezi Februari mwakani, upo utaratibu unaofanywa ili kuwezesha walimu wao kuwafundisha maeneo ambayo watakuwa hawajasoma.
Pia serikali imewaagiza wakuu wote wa shule nchini kuchukua hatua za haraka na watoe taarifa kwa viongozi wa Halmashauri za Wilaya na Mikoa pindi wanapogundua dalili za mgogoro ili hatua zichukuliwe.

Alisema wanafunzi wanapaswa kufuata njia halali kufuatilia mahitaji yao.
Kuhusu suala la udini kama lilivyotajwa awali kuwa ni sehemu ya mgogoro huo. Bhalalusesa alisema wizara yake haiwezi kukataa au kukubali kwa sababu ndani ya shule hiyo kulikuwa na uhuru na utovu wa nidhamu uliopitiliza hadi ilifikia mwaka jana mmoja wa walimu shuleni hapo kubakwa.
Kuhusu utoro wa walimu, Bhalalusesa alisema baadhi yao wanakaa Dar es Salaam hivyo hutumia kama kisingizio.
                                     CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment