Pages

Friday, December 28, 2012

Sheikh Dar alaani padri kupigwa risasi.

SIKU moja baada ya padri wa kanisa Katoliki lililoko Mpendae visiwani Zanzibar, Ambrose Mkenda, kujeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake wakati akitoka kanisani, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, amelaani tukio hilo na kuwataka Watanzania kuwafichua wale wote waliohusika katika tukio hilo baya kwa mustakabali wa taifa.

Akizungumza  jana, Sheikh Salum alisema hivi sasa kumekuwa na viashiria vinavyonekana kutaka kutowesha amani, jambo linalohitaji kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha amani inaendelea kudumu.

Alisema ni muhimu Watanzania wakawafichua wale wote waliohusika katika tukio hilo, ili kujua ukweli na kuweza kulisaidia Jeshi la Polisi.

“Ni muhimu kujua ukweli wa tukio hili, kwani wapo wanaoweza kuamini kuwa ni viashiria vya chuki vya kidini,” alisema.

Alisema mauaji ya kimbari yaliyojitokeza katika baadhi ya nchi nyingine za Afrika yalichangiwa na vitu mbalimbali ikiwemo matatizo ya udini, ukabila vitu ambavyo vimeanza kujitokeza nchini.
Sheikh Salum alisema mfumo wa kukubali ukabila huku wengine wakinyimwa haki inaweza kuwa chanzo cha kutokea kwa vurugu, hivyo kuna haja ya kushirikiana kwa umoja, ili kukomesha viashiria hivyo.

No comments:

Post a Comment