Pages

Thursday, January 31, 2013

Mbunge Mpanda Mjini akerwa na majibu ya mawaziri

MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA) amewashambulia mawaziri wa Wizara ya Uchukuzi kwa madai kuwa wanatoa majibu ambayo hayakidhi viwango.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akiuliza maswali ya nyongeza kwa kuitaka serikali itoe majibu ya kuwaeleza Watanzania hususani wa Mpanda ni kwanini stesheni ya eneo hilo haina nyumba ya kusubiria gari moshi (treni) wala choo.

Mbunge huyo pia aliitaka serikali ieleze ni lini safari za garimoshi zitaanza kutolewa kila siku ili wananchi waepukane na usumbufu wa kuuziwa tiketi kwa kulanguliwa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Sabrina Sungura (CHADEMA) alitaka serikali kutoa kauli bungeni ni lini itajenga jengo la stesheni ya reli Kigoma kutokana na jengo hilo kuwa katika hali mbaya na linaweza kuanguka muda wowote.

Mbunge huyo alisema kuwa licha ya kuwa Kigoma ni sehemu ya kihistoria kwa kutumia stesheni hiyo, lakini cha ajabu jengo hilo linavuja.
Awali katika swali la msingi, Arfi alitaka kujua ni lini serikali itajenga jengo la Shirika la Reli lenye hadhi katika stesheni ya reli Mpanda.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, alisema serikali ina nia njema ya kuboresha miundombinu ya shirika hilo yakiwemo majengo ya stesheni zote nchini.
Tizeba, alisema kuwa, kwa sasa serikali inatafuta fedha ili kuhakikisha wanajenga kituo cha stesheni ya Kigoma ili kuendelea kukifanya kuwa cha kihistoria.

No comments:

Post a Comment