Pages

Tuesday, January 29, 2013

Msajili amkwamisha Elizabeth Michael ‘Lulu’,hadi leo

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilimpa masharti matano ya dhamana msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba.
 Masharti hayo yaliyolewa na Jaji Zainabu Mruke, muda mfupi baada ya mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe, kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mteja wao ambaye amekuwa akisota rumande tangu Aprili mwaka jana. 

Mawakili hao walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha 148(1), (2) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .
Jaji Mruke alisema, ili mahakama impatie dhamana msanii huyo, ni lazima asalimishe kwa Msajili wa Mahakama hiyo hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi, kuwa na wadhamini wawili watumishi wa serikali, ambao watasaini bondi ya sh milioni 20 kila mmoja.

Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo, Lulu na wakili wake walitoka nje ya ukumbi uliokuwa ukiendeshwa shauri hilo kwa ajili ya kwenda kwa msajili kutimiza masharti hayo, lakini bahati mbaya hakuwepo ofisini, hivyo kumfanya Lulu kurudishwa rumande hadi leo, atakapoletwa kwa ajili ya kutimiza masharti hayo mbele ya msajili wa mahakama hiyo.
Licha ya mahakama hiyo kumpatia masharti ya dhamana Lulu, kutokana na ombi lake Na.125/2012, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili, ambayo ni ya kuua bila kukusudia, haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Desemba 21, mwaka jana, Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi ya kuua bila kukusudia ya Lulu na kuihamishia rasmi Mahakama Kuu na uamuzi huo ulitokana na upande wa jamhuri kumsomea maelezo ya kesi yake kwa kina na kuieleza mahakama kuwa wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi tisa.

No comments:

Post a Comment