Pages

Wednesday, January 23, 2013

Mwaitege kupamba uzinduzi wa Baraka Huja

MWIMBAJI mahiri wa nyimbo za injili nchini, Bony Mwaitege, anatarajiwa kuupamba uzinduzi wa albamu ya ‘Baraka Huja’ ya Baraka Legembo, utakaofanyika ndani ya Kanisa la Pentecoste Holiness Mission lilipo Changanyikeni jijini Dar es Salaam, Januari 27, mwaka huu.

Akizungumza  jana, Legembo alisema kuwa Mwaitege amekubali kuimba katika uzinduzi huo unaotarajiwa kuanza majira ya saa 7:00 mchana mara baada ya ibada.
“Mwaitege amekubali kuja kwenye uzinduzi wa albamu yangu, hivyo nawaomba wakazi wote wa Changanyikeni kufika kwa wingi katika shughuli hiyo itakayoanza saa 7:00 mchana, mara baada ya ibada,” alisema Legembo.

Legembo aliwataja waimbaji wengine watakaoimba siku hiyo kuwa ni kwaya wenyeji, Elshadai Aliko Mwandelile, Ipyana Wasoto, Linus, Hanston, Eliza, Neema, Kwaya ya Lulu na Mount Herob.
Aidha, alisema kuwa lengo la uzinduzi huo ni kupata fedha ambazo zitamsaidia katika kurekodi albamu hiyo katika mfumo wa video, kwani watu wengi wamekuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.

“Lengo la kuzindua albamu yangu ni kupata fedha ambazo zitanisaidia kurekodi albamu hii katika mfumo wa video, kwani watu wengi wamekuwa wakiiulizia kila ninapokwenda kuhudumu,” alisema Legembo.
Aliongeza kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo atamtangaza siku za hivi karibuni, hivyo wadau wote wafike bila kukosa.

No comments:

Post a Comment