Pages

Wednesday, January 2, 2013

RITA: Wananchi wengi kupata vyeti vya kuzaliwa 2013.

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), amepanga kutoa vyeti vingi vya kuzaliwa kwa wananchi ndani ya mwaka 2013.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Phillip Saliboko, katika taarifa yake ya salamu za Mwaka Mpya.

Saliboko amewataka wananchi kufika katika ofisi za wakala huyo ili kupata huduma hiyo ambayo imeboreshwa na kwa kipindi kifupi unapata cheti tofauti na ilivyokuwa awali.

“RITA tunatoa huduma zipatazo 17 kwa wananchi kubwa likiwa ni usajili wa vizazi na vifo ambao hupatikana makao makuu na katika wilaya zote nchini…kimsingi tumejitahidi kwa mwaka uliopita kuwahudumia wananchi wetu vizuri na tunaahidi kufanya maboresho ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema.

Alisema moja ya mikakati yao ni kufanya kampeni za usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa katika wilaya 12 huku wakipita kila kata za wilaya ambazo zitachaguliwa hatua itakayosaidia wananchi wengi zaidi hasa wa maeneo ya vijijini kupata vyeti hivyo.

“Tunawashukuru viongozi wote katika wilaya tulizofanya kampeni kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia na kufanikisha mikakati hii na kwa mwaka mpya wa 2013 tunakusudia kuimarisha mpango huu na kuutekeleza katika wilaya nyingi zaidi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Saliboko.

Saliboko alisema kuwa mkakati mwingine ni pamoja na kuanza kusajili watoto walio na umri chini ya miaka mitano (Under Five Birth Registration Initiative – U5BRI) ambao utekelezaji rasmi unategemewa kuanza mkoani Mbeya Aprili mwaka huu.
Alisema kuwa katika mkakati huu watoto walio na umri huo watasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bila malipo katika ofisi za watendaji kata na katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya afya ya mtoto.

Saliboko alisema kuwa RITA inategemea pia kutoa huduma za usajili katika taasisi na mashirika na kuzipa uwezo zaidi ofisi zake za wilaya katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za wakala.

No comments:

Post a Comment