Pages

Wednesday, January 30, 2013

Serikali yatafakari kiburi cha makampuni ya simu

SERIKALI imeahidi kuanza kutafakari juu ya suala la makampuni ya simu ambayo hayataki kupeleka huduma hiyo katika maeneo yote ambayo hayana mawasiliano ya simu kwa kuwapunguzia masafa.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) aliyetaka kujua mpango wa serikali katika kuyalazimisha makampuni hayo ya simu kupeleka huduma hiyo katika maeneo yasiyo na simu.

“Serikali itaanza kutafakari suala hili kwa kina ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya ama kuwapunguzia masafa makampuni haya ya simu katika maeneo yote ya hapa nchini yasiyo na umeme,” alisisitiza Makamba.

Katika swali lake mbunge huyo alihoji kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) bado kumekuwepo na ahadi nyingi toka serikalini kuwa, wanafanya upembuzi yakinifu, wapo katika mchakato, lakini hadi sasa hakuna hata mnara mmoja uliojengwa katika maeneo ambayo hayana umeme, hususani kwa Jimbo la Manyovu na hivyo kutaka kauli ya serikali.

Katika swali la msingi la Mbunge wa Manyovu, Albert Ntabaliba (CCM) alitaka kujua ni lini Tarafa ya Muyama katika Jimbo la Manyovu itawekewa mnara wa mawasiliano, na lini serikali itafika Manyovu kuona hali ilivyo, ikilinganishwa na minara iliyopo upande wa Burundi wakati upande wa Tanzania hakuna minara.
Akijibu swali hilo, Makamba alisema serikali kupitia UCAF tayari imekwishachagua kampuni ya simu itakayopeleka mawasiliano katika Tarafa ya Muyama.
Alibainisha kuwa wizara yake imetenga ruzuku ya jumla ya dola za Kimarekani 173,000 kwa ajili hiyo na kwamba kazi hiyo inatarajiwa kuanza kabla ya Machi mwaka huu.

No comments:

Post a Comment