Pages

Saturday, January 26, 2013

Simba yamkera NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, amekerwa na kitendo cha uongozi wa timu ya Simba kupanga nyota chipukizi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, juzi.

Katika mechi hiyo iliyoisha kwa Simba kufungwa bao 1-0, hakuna nyota hata mmoja wa kikosi cha kwanza aliyepangwa, licha ya mashabiki kuwa na shauku ya kukiona kikosi cha Simba kilichorejea hivi karibuni kutoka kambini nchini Oman.
Waziri Makalla alisema, kitendo hicho hakipaswi kufumbiwa macho, kwani kinawakatisha tamaa mashabiki, akiwemo yeye ambaye alikuwepo, waliokwenda uwanjani kuwaona Simba, lakini wakaishia kuwaona ‘chekechea’ kwenye mechi hiyo.

Alisema jambo hilo lina athari kubwa katika mustakabali wa soka nchini, kwani linawavunja moyo mashabiki, hivyo siku nyingine kutojitokeza uwanjani kwa hofu ya kuingizwa mkenge.
“Kama mashabiki walielezwa ni mechi ya Simba na Black Leopard, walipaswa kuiona Simba ikicheza, sio kikosi cha pili kama ilivyokuwa jana,” alisema Makalla.
 
Alisema kitendo hicho hakipaswi kufumbiwa macho, kwani sio tu hakiwatendei haki wapenzi na mashabiki, bali pia siku nyingine watasita kujitokeza viwanjani kushuhudia mechi za kirafiki, kitu ambacho si kizuri kwenye soka.
Mbali ya waziri kukerwa na kitendo hicho, hata mashabiki wa Simba na Yanga waligubikwa na hasira mara baada ya kuona kikosi cha vijana cha Simba kikitua dimbani kuwakabili Black Leopards, ikiwa ni nje ya makubaliano ya mchezo huo.

Baada ya kikosi hicho kuingia uwanjani, mashabiki walianza kuwaponda na kuwazomea viongozi wa Simba, wakidai ni wababaishaji na kwenda mbali zaidi kwamba ni sawa na kamari ya mitaani, ambayo sawa na wizi wa wazi, kwani walitarajia kuiona Simba ya Oman.
Shabiki Juma Saidi alisema, kitendo kilichofanywa na uongozi wa Simba kimemsikitisha, kwani akiwa mpenzi wa timu hiyo, alikwenda uwanjani na kulipa kiingilio kwa lengo la kuishuhudia Simba ikicheza baada ya maandalizi ya Oman.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Simba, lakini kitendo cha viongozi wetu kuchezesha kikosi cha watoto wakati sisi tulitegemea kuona kikosi cha Oman tuone maandalizi ya huko, kama ni hivyo waendelee kuwachezesha hao hata Ligi Kuu,” alisema shabiki huyo.
Mwingine ni Chalz Baba, Rais wa Bendi ya Mashujaa, aliyesema kuwa amekerwa na kitendo hicho, kwani alikwenda kuwaona Simba waliotoka Oman sio vijana.
Katika mechi hiyo, Simba iliwakilishwa na Abuu Hashim, William Weta, Emiry Mgeta, Hassan Isihaka, Hassan Hatib/Haruna Shamte, Saidi Ndemla, Ramadhan Singano, Ibrahim Ajid, Marid Kaheza, Rashid Ismail, Miraji Kadenge.

No comments:

Post a Comment