Pages

Wednesday, January 2, 2013

Trafiki yatangaza vituo maalumu vya ukaguzi.

KIKOSI cha Usalama Barabarani Nchini, kimetangaza kuanzisha vituo maalumu vya ukaguzi wa mabasi ya abiria badala ya utaratibu inaoutumia sasa wa kuyakagua kila sehemu.

Hatua hiyo ilitangazwa juzi usiku jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Mohamed Mpinga, wakati akizungumza katika Televisheni ya Taifa (TBC).

“Tuna mikakati minne tuliyojiwekea kwa mwaka 2013; tuna mpango wa kufanya ukaguzi kwa mabasi ya abiria kwa kuweka vituo maalumu badala ya kuyasimamisha kila sehemu. Kwa kaskazini tutaweka pale Same, kwa kwenda njia ya kati tutaweka Singida na kwenda kusini tutaweka kituo mkoa wa Iringa,” alisema Kamanda Mpinga.

Alieleza kuwa kwa mwaka huu wamejipanga ipasavyo kuboresha mifumo ya utendaji kazi eneo ambalo litahusisha ukaguzi wa magari kwa lazima ambapo magari hayo yatakaguliwa kwa kina.

Alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kutumia vifaa vya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kufanikisha hilo wamekuwa wakifanya mazungumzo mbalimbali na wadau hao ili kufanikisha matumizi ya vyombo hivyo.

Jingine ni kufanya utambuzi wa maeneo hatarishi kama mbinu za kupunguza ajali za barabarani akatolea mfano kwa mkoa wa Pwani ambao waliufanya kama eneo la mfano kwa kuweka vidhibiti mwendo kasi na mafanikio wameyaona.

Alisema hatua hiyo imewezesha ajali kwa mkoa wa huo kupungua kwa asilimia 37, vifo kwa asilimia 57 na majeruhi kwa asilimia 48 ikilinganishwa na mwaka juzi.

No comments:

Post a Comment