Pages

Sunday, January 27, 2013

Wanane wafariki, 300 hoi kwa kipindupindu Rukwa

WATU wanane wamekufa na wengine 300 hoi kutokana na kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo uliovikumba vijiji na kambi za wavuvi katika Bonde la Ziwa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Ugonjwa huo ulijitokeza kwa mara ya kwanza tangu Novemba mwaka jana. Mikusanyiko ya aina yoyote imepigwa marufuku katika eneo hilo ikiwamo minada , unywaji pombe za kienyeji na serikali inawahimiza wakazi wa maeneo hayo kuhakikisha wanachimba vyoo na kuvitumia.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Thomas Rutayazibwa amethibitisha kutokea kwa mlipuko huo, wagonjwa wapatao 300 wamekuwa wakitibiwa katika kambi mbalimbali zilizoanzishwa rasmi kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa kipindupindu, huku wengi wakielezwa kuwa hali yao ilikuwa mbwaya sana walipofikishwa kwa mara ya kwanza.
Aliongeza kuwa kambi za uvuvi zikiwemo Nkwiro , Kalumbaleza , Nankanga, Ilemba na kijiji cha Muze ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika kwa mlipuko wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dk Rutayazibwa, baadhi ya vyanzo muhimu vya maji vikiwemo Mito Nkwilo na Kalumbaleza vimeharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo za wakazi wa maeneo hayo kuoga katika mito hiyo hivyo kusababisha uchafuzi wa maji yake ambayo kitabibu hayafai tena kwa kunywewa bila kuchemshwa .
“Ili kukabiliana na kutoendelea kuenea kwa ugonjwa huo tayari tumeshaanza kuwaelimisha wakazi wa maeneo hayo njia bora za kujikinga nao ikiwemo kutokula viporo vya chakula bila kuchemsha, pia matumizi ya vyoo.
“Lakini kubwa tulichobaini ni kwamba maeneo mengi katika eneo hili la Bonde la Ziwa Rukwa hawana vyanzo vya uhakika vya maji.
“Kwa kweli vyanzo hivi si salama kwa matumizi ya binadamu hivyo tumechukua sampuli ya maji hayo kwa ajili ya kuyapeleka kwa mkemia kwa uchunguzi wa kitaalamu, huku kwa sasa tunawahimiza wachemshe maji kabla ya kuyanywa,”alisema.
Hata hivyo alianisha changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo katika kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo ikiwemo viongozi wa Serikali za vijiji katika Bonde hilo la Ziwa Rukwa kutohamasisha wakazi wa maeneo hayo kanuni za bora za afya kwa dhana kwamba ni jukumu la Serikali ya Wilaya.

No comments:

Post a Comment