Pages

Monday, February 25, 2013

Maskini Simba...Yalala kwa Mtibwa, vurugu kubwa zaibuka Taifa

KAMA ni mtoto, unaweza kusema si riziki. Hivi ndivyo hali ilivyo ndani ya klabu ya Simba, ambako imeendelea na mwenendo wa shaka katika Ligi Kuu Tanzania bara, baada ya jana kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wakata miwa wa Mtibwa Sugar kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo, msimu huu imekuwa na mwenendo mbovu na hata kufuta mawazo ya kutetea taji hilo miongoni mwa mashabiki wake, ambao hivi sasa wako katika hali mbaya kutokana na kufanya vibaya.
Hadi sasa, Simba imepoteza mechi tatu huku ikijikongoja katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 18. Yanga wako kileleni kwa pointi 39 huku Azam ikifuatia kwa pointi 36.

Katika mechi ya jana, Simba ilianza kwa kasi na dakika ya tatu tu, Shomari Kapombe alipokea pande la Amir Maftah, lakini shuti lake likaokolewa na kipa Hussein Sharrif, kabla ya Mtibwa kujibu mashambulizi na kupata kona ambayo haikuzaa matunda.
Alikuwa ni Salvatory Ntebe dakika ya 16, aliyeiandikia Mtibwa bao hilo la pekee, baada ya kuunganisha mpira uliotokana na kona.

Dakika ya 41, Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na nafasi yake kuchukuliwa na Kigi Makasi.

Redondo baada ya kutoka alikwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya kuvalia badala ya benchi la wachezaji wa akiba. Kitendo kama hicho kilifanywa na Haruna Moshi ‘Boban’ siku walipocheza na Libolo kwenye uwanja huo.
Hadi mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga akiashiria mapumziko, Mtibwa walikuwa mbele kwa bao hilo.

Kipindi cha pili, Simba walirejea kwa nguvu na dakika ya 49, shuti la Haruna Chanongo lilipaa langoni mwa Mtibwa sentimita chache.
Simba walifanya mabadiliko tena dakika ya 51, kwa kumtoa Boban na nafasi yake kuchukuliwa na Amri Kiemba, ambako kabla ya kutoka, alimkumbatia Kigi Makasi na kama mazoea yake, alikwenda moja kwa moja vyumbani.

Dakika ya 86, Simba ilipata pigo, baada ya Juma Nyoso kulimwa kadi nyekundu kutokana na kumkwatua Vicent Barnabas wakati mpira ukiwa umetoka nje. Hadi Mwamuzi Kidiwa akimaliza mpira, Mtibwa iliibuka kidedea kwa bao 1-0.

Matokeo hayo yaliibua vurugu miongoni mwa mashabiki wa Simba, ambao walitaka kuvamia jukwaa kuu kuwashughulikia baadhi ya viongozi waliokuwepo.
Kutokana na hali hiyo, polisi iliwalazimu kufunga baadhi ya njia za kuingilia maeneo ya jukwaa kuu ili kuwanusuru viongozi hao, hali ambayo ilisababisha adha kubwa kwa mashabiki wakati wa kutoka.

Lakini mashabiki hao wa Simba, walibaki nje ya uwanja wakiwa katika vikundi vikundi, hali iliyosababisha wachezaji kufungiwa vyumbani. Mashabiki hao walisikika wakiutupia lawama uongozi huku wakidai hawamtaki kocha, Mfaransa Patric Liewig.
Hali ilizidi kuwa mbaya, ambako Uwanja wa Taifa uligeuka uwanja wa vita, baada ya polisi kulazimika kutumia maji ya kuwasha kuwatawanya mashabiki hao, huku basi la Simba likiondoka likisindikizwa kwa ulinzi wa hali ya juu.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Amir Maftah, Juma Nyoso, Komanbil Keita, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’/Amri Kiemba, Haruna Chanongo/Mrisho Ngasa, Ramadhani Chombo ‘Redondo’/Kigi Makasi.
Mtibwa: Hussein Sharrif, Said Mkopi, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Salvatory Ntebe, Salum Swedi, Shabani Nditi, Jamal Mnyate,  Hussein Javu/Juma Liuzio, Shabani Kisiga ‘Malone’, Rashid Gumbo, Vicent Barnabas.

No comments:

Post a Comment