Pages

Thursday, February 28, 2013

Meya CCM Bukoba atoswa

MGOGORO ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba Mjini, unazidi kuchukua sura mpya baada ya madiwani wake tisa kuungana na wenzao wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) na wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukwamisha kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kiketi jana kujadili bajeti ya 2014/2014.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya madiwani 10 wa Halmashauri ya Mji wa Bukoba akiwemo Mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagesheki kutukanwa matusi ya nguoni kupitia vipeperushi vilivyosambazwa mjini humo na watu wasiojulikana.

Madiwani waliotukanwa matusi hayo mazito ni nane wa CCM na wawili wa CUF waliosaini hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani ili kumng’oa Meya Anatory Amani anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Halmashauri hiyo ina madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM. Ili kikao cha baraza kiweze kuendelea ni lazima akidi ya mahudhurio iwe na nusu ya wajumbe jambo ambalo lilishindikana jana.

Wakizungumza kutoka mjini Bukoba, baadhi ya madiwani walisema kuwa Meya Amani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kagondo, alipata wakati mgumu hadi kulazimika kukiahirisha kikao hicho.
Kwamba muda wa kuanza kikao ulipowadia, ukumbini walikuwemo wajumbe 11, yaani madiwani nane wa CCM, wawili wa CHADEMA na mmoja wa CUF, jambo lililomlazimu meya huyo kuwapigia simu baadhi ya wale ambao walikuwa hawajafika na kuwashawishi bila mafanikio.

“Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Zipora Pangani naye aliingilia kati kumsaidia meya kiasi cha kufikia hatua ya kuwapigia simu madiwani hao, kila mmoja akimbembeleza ataje mahali alipo ili amtumie gari imchukue au kitabu cha mahudhurio asaini huko aliko, lakini ilishindikana,” alisema mmoja wa madiwani.
Habari zaidi zinasema kuwa, Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera naye aliingilia kati kwa 

kumwagiza katibu wa wilaya awatafute madiwani wa chama hicho ambao hawakuwa ukumbini, lakini haikuwezekana kwani simu zao zilikuwa zimefungwa.
Baada ya kuona hali inakuwa tete, Meya Amani alikiahirisha kikao kwa muda hadi saa 6:30 mchana ingawa hali iliendelea kubakia vile vile, na hivyo ukafikia uamuzi wa kusitisha baraza hilo hadi Machi 1 na 2 mwaka huu.

Akiahirisha kikao hicho, Meya Amani kwa hasira alisema kuwa madiwani hao waliokwepa wanapaswa kupigwa mawe na kulaaniwa kwa kukwamisha maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo, tarehe hizo zilizopangwa kufanyika baraza hilo zimezua utata kwani zilishapangiwa shughuli nyingine ya vikao vya kujadili utekelezaji wa bajeti ya robo mwaka ya pili ya 2012/2013.

Ni dhahiri kuwa mgogoro huo unazidi kukimega chama kwani Meya Amani kwa upande mwingine amepuuza maagizo ya Makamu Mwenyekiti CCM Taifa, Philip Mangula kwa kuamua kufungua kesi mahakamani kupinga kujadiliwa na kung’olewa na madiwani.
Mangula ambaye alilazimika kufika mjini Bukoba mwezi uliopita ili kunusuru mtafaruku huo, aliagiza madiwani nane wa CCM waliokuwa wamesaini hati hiyo, waondoe tuhuma hizo na kuzipeleka kwenye chama ili zipatiwe ufumbuzi.

Madiwani waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya huyo mbali na Kagasheki ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Kata ya Buhende) na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Bukoba.

Wengine ni Richard Gasper (Miembeni), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe) na Mulubi Kichwabuta (Viti Maalumu) na wale wa CUF ni Ibrahim Mabruk (Bilele) na Rabia Badru wa Viti Maalumu.
Taarifa kutoka mjini Bukoba zilisema kuwa madiwani hao nane wa CCM, jana waliandika barua ya malalamiko kwenda kwa katibu wa chama hicho wilaya na nakala zake kwa Mwenyekiti wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa na Mangula.

Juzi, madiwani nane wa CCM walikabidhi barua kwa Katibu wa Wilaya wakipinga kushiriki vikao vyote vitakavyoongozwa na Meya Amani wakimtuhumu kuwa ndiye alihusika kusambaza vipeperushi vya kuwakashifu.
Katika vipeperushi hivyo, madiwani hao kila mmoja alitajwa kwa jina lake, kata na orodha ya tuhuma zake huku wengine wakidaiwa kulaghaiwa kwa fedha na mmoja wa viti maalumu akidhalilishwa kwa tuhuma za ngono.

Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na madiwani wenzake kadhaa wa CCM, waliwasilisha barua zao kwa mkurugenzi ili kuondoa tuhuma zao kwa muda asubuhi ya Januari 23 mwaka huu, lakini mchana wa siku hiyo Meya Amani akafungua kesi ya kupinga asijadiliwe.
Mangula aliwataka madiwani hao kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe ingawa mkuu huyo pamoja na Pangani, Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wanadaiwa kumkingia kifua Amani.
Madiwani hao wanapinga mikataba ya miradi mikubwa miwili ya uuzwaji wa viwanja zaidi ya 5,000 na ujenzi wa soko la kisasa wakidai imasainiwa kifisadi kwa siri na Meya Amani.

No comments:

Post a Comment