Pages

Monday, March 25, 2013

Walimu kuitikisa upya serikali

Akizungumza  Jumamosi jijini Dar es Salaam, jana,  Rais wa CWT, Gratian Mkoba, alisema endapo serikali haitaidhinisha madai yao ni lazima moto uwake  kwani wamechoka kufanya kazi katika mazingira magumu na kudharauliwa.
                                                 Rais wa CWT, Gratian Mkoba.
Chama cha Walimu nchini (CWT) kimetishia kuwasha moto mpya iwapo serikali itaendelea kupuuzia madai ya stahili zao.
Hayo ameyabainisha wakati kamati  ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ikichunguza sababu za wanafunzi kufanya vibaya kwenye mtihani wa kidato cha nne  mwaka jana na kusisitiza kuwa hawatafuata sheria na 'patachimbika'.
 
Alisema endapo bajeti ya mwaka huu itapita bila kutekeleza ahadi za nyongeza ya mishahara ya  walimu kama walivyokubaliana siku za nyuma, hawatakuwa na sababu za kufuata utawala wa sheria wala chochote kwa kuwa serikali yenyewe haifuati sheria.
 
“Huu utakuwa ni mgogoro mpya endapo bajeti ya mwaka huu itapita bila kuongeza mishahara ya walimu ni lazima moto utawaka na wabunge waiulize serikali madai ya walimu yamefikia wapi na tutaendelea kuteseka hadi lini,” alisema. 
 
Aliwataka wabunge kuiuliza serikali juu ya nyongeza ya mshahara wa walimu ikiwa ni jitihada za kuboresha elimu nchini.
 
Kuhusu Kamati ya Pinda, ana hofu kuwa serikali ina nia mbaya na walimu kwani kitendo cha hivi karibuni cha kuunda kamati ya Waziri Mkuu bila kutaja chochote juu ya kuchunguza marupurupu na nyongeza ya mishahara ya walimu kunawaacha vinywa wazi.
 
Mkoba alisema madai yao sio mapya yanafahamika na kwamba kama serikali imeyasahau watarudi mahakamani kuikumbusha.
 
Alisema Agosti mwaka jana walifanya mgomo wa kutaka nyongeza ya mshahara ifikie asilimia 100, posho ya kufundishia asilimia 55 kwa walimu wa sayansi na wa sanaa ifikie asilimia 50. Kingine ni asilimia 30 ya  posho ya mazingira magumu jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezwa.
 
Mkoba alisema shauri lao lilipelekwa mahakamani na kuamulikwa kuwa  serikali pamoja na walimu wake  kulijadili lakini serikali haijawahi kukubaliana na hatua  hiyo licha ya kwamba mwisho wa kulijadili kisheria suala hilo ilikuwa  Desemba 5 mwaka jana.
 
Ukosefu wa walimu, upungufu wa vitabu na mazingira duni ya kujifunzia ni baadhi ya sababu zilizotolewa na wadau wa elimu waliohojiwa na tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012

No comments:

Post a Comment