Pages

Friday, April 26, 2013

Mbunge akerwa na majibu ya waziri.

MBUNGE wa Viti Maalumu, Dk. Pudenciana Kikwembe (CCM) ameeleza kukerwa na majibu ya Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi, Philipo Mulugo yasiyotoa majibu ya kina kuhusu walimu kukatwa asilimia mbili ya mshahara.

Kikwembe alitoa kauli hiyo bungeni jana alipouliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali ieleze ni kwa sababu gani walimu wamekuwa wakikatwa fedha hizo bila kushirikishwa.

“Mheshimiwa spika napenda kusema nasikitishwa na majibu ya naibu waziri kwa kushindwa kutoa majibu ambayo ni ya uhakika, si kweli kuwa walimu wanaokatwa asilimia mbili ya mshahara wao wanakuwa wameshirikishwa, hata mimi nilikuwa mwalimu, nilikuwa nikikatwa, lakini sijawahi kushirikishwa,” alisema Dk. Kikwembe.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alisema walimu wanakatwa asilimia mbili ya mishahara kwa ajili ya kuchangia Chama cha Walimu Tanzania (CWT), lakini wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.

Kutokana na hali hiyo, alihoji ni kwanini chama hicho hakioni umuhimu wa kuwapatia walimu mikopo isiyokuwa na riba kama vile ujenzi wa nyumba, ili kuwakwamua katika mazingira magumu ya kimaisha.

Akitolea ufafanuzi wa swali la nyongeza la Dk. Kikwembe, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alisema kwa sasa ametoa agizo kwa waajiri kutowakata asilimia mbili ya mishahara walimu ambao ni ajira mpya hadi hapo watakapopatiwa elimu juu ya makato hayo.
Kwa upande wake, Mulugo akijibu swali la msingi alisema kwa sasa CWT kipo kwenye hatua za mwisho za kufungua Benki ya Walimu ambayo itaanza kufanya kazi Juni mwaka huu.
Alisema benki hiyo itakapoanza kila mwalimu atakuwa na haki ya kukopa kwa ajili ya mahitaji yake kama vile kujenga nyumba, kusomesha, watoto wao ama kujisomesha wao wenyewe.

No comments:

Post a Comment