Pages

Wednesday, April 24, 2013

Mwenyekiti wa Bunge aburuzwa kwa Spika,Wabunge wanawake CHADEMA wadai aliwadhalilisha.

KAULI ya Mbunge wa Uzini, Mohammed Seif Khatib (CCM) kwamba wabunge wa viti maalumu CHADEMA wamepata nafasi hizo kwa vile ni wake, wapenzi na wachumba wa viongozi wa chama taifa, imesababisha wabunge hao kuvamia ofisi ya Spika kushitaki, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Wabunge hao pia walilalamika kauli ya udhalilishaji iliyotolewa hivi karibuni bungeni na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) kwamba baadhi ya wabunge wanapata mimba zisizotarajiwa.

Khatib alitoa kauli hiyo ya udhalilishaji mjini Morogoro katika mkutano wa hadhara wa CCM uliowashirikisha viongozi wa kitaifa akiwemo Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Habari  zilisema kuwa wabunge hao walifika katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda juzi na kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya kauli ya Khatib.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa wabunge hao walishangazwa na kauli ya Khatib ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge, kusaidia shughuli za Bunge pale spika au naibu wake wanapokuwa hawapo.

“Hii kauli ni mwendelezo wa vitendo vya udhalilishaji kwa wabunge wanawake vinavyofanywa na wabunge wanaume, na kibaya zaidi kauli hiyo safari hii imetolewa na Mwenyekiti wa Bunge,” alisema mmoja wa wabunge hao waliokwenda kwa spika.
Walimtaka Khatib awaombe radhi vinginevyo watachukua hatua zaidi kupinga udhalilishaji huo.

Akijibu malalamiko ya wabunge hao, Makinda aliungana nao kwa kusema kauli za Khatib na Lusinde hazipaswi kufumbiwa macho kwani ni dhahiri zimewadhalilisha wabunge wanawake.

“Kwa wanawake wenye hadhi ya ubunge, huwezi kusema wanapata mimba za bila kutarajia na hii isiwafanye muone aibu kuzaa.

“Hata kama hujaolewa huna sababu ya kuona aibu kwamba utaambiwa umepata mimba ya bila kutarajia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Makinda alisema serikali inakamilisha ujenzi wa jengo moja ndani ya eneo la Bunge ambalo litakuwa kwa ajili ya wabunge wajawazito na wenye watoto wachanga.

Kwa mujibu wa Spika Makinda, mbunge mwenye mtoto mchanga ataruhusiwa kuja na wasichana wa kazi ambaye atakaa kwenye jengo hilo wakati vikao vya Bunge vikiendelea.
“Kwa hiyo kama unataka kunyonyesha mtoto, unatoka ukumbini, unaingia kwenye jengo hilo unanyonyesha, ukimaliza unarudi bungeni kuendelea na kazi,” alisema.
Katika mkutano huo wa CCM, ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni ya Taifa, Khatib ambaye pia ni Katibu wa Oganaizesheni ya chama hicho, alisema CHADEMA ina wabunge wa kuchaguliwa na viti maalumu.

Alifafanua kuwa ukiacha wale wa kuchaguliwa, wabunge wa viti maalumu walipatikana kutokana na kuwa wachumba, wake na wapenzi wa viongozi wa CHADEMA Taifa.
Khatib huku akifahamu wazi kuwa wabunge hao wamepatikana kwa utaratibu wa kikatiba ambao umeidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), aliongeza kuwa CHADEMA inaongozwa na wazinzi wenye dhambi wasiofaa kwenda Ikulu.
Hivi karibuni baada ya baadhi ya wabunge wa CCM akiwemo Lusinde kuibua matusi kwa wanawake, Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) aliwataka wabunge wanawake kwa niaba ya wanawake wengine wakatae vitendo hivyo.
Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wabunge Wanawake (Ulingo) pia alielezwa kukerwa na mifano ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) aliyenukuu maandiko ya Biblia Takatifu, yasemayo “mwanamke mpumbafu huivunja ndoa yake mwenyewe”.

No comments:

Post a Comment