Pages

Saturday, April 27, 2013

Wanafunzi washikiliwa polisi.

JESHI Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia wanafunzi watano wa Shule ya Sekondari ya Mizengo Pinda iliyopo Kata ya Kibaoni Wilaya ya Mlele kwa tuhuma za kuwaongoza wanafunzi wenzao kufanya vurugu.

Katika vurugu hizo, wanafunzi hao wanadaiwa kuharibu majengo ya shule na kisha kumjeruhi mwalimu wao wakimtuhumu yeye na mkuu wa shule hiyo kuwa walimloga mwanafunzi mwenzao akawa na ugonjwa wa mapepo.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Emanuel Nley aliwataja wanafunzi waliokamatwa kuwa ni Isaya Benezeti (18),Aloyce Nshaki (17),Coaster Petro (19), John Salumu (19) na January Sanane (20) wote wa kidato cha nne.

Alisema kuwa siku ya tukio Aprili 21, mwaka huu, saa 2:30 usiku, watuhumiwa hao waliwaongoza wanafunzi wenzao kuharibu jengo la utawala kwa mawe na matofali kisha kuvunja mlango na madirisha.

Nley aliongeza kuwa baada ya kuharibu jengo hilo, wanafunzi walikwenda nyumbani kwa mkuu wa wa shule, Alko Kaminyoge, wakimtuhumu pamoja na mwalimu wa taaluma, Boniface Salamba, kujihusisha na ushirikina.
Aliongeza kuwa baada ya hapo walivamia nyumba ya Mwalimu Boniface na kufanya vurugu kisha walimshambulia kwa mawe na kumsababishia maumivu sehemu mbalimbali za mwili.
Kamanda alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

No comments:

Post a Comment