Pages

Saturday, April 27, 2013

Wawili mbaroni kwa kumuua mwenzao.

JESHI la Polisi Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi linawashikilia  watu wawili wakazi wa Kijiji cha Igalila Kata ya Mpanda Ndogo, Tarafa ya Kabungu  kwa tuhuma  za kumuua mwenzao, Rehani  Pesambili (70), kwa kumpiga mateke na ngumi wakati wakinywa pombe ya kienyeji aina ya komoni.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Emmanuel Nley,  aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Geofrey Pesambili  (24) na Efram Adamu ( 28) .

Alisema  tukio hilo  lilitokea Aprili 20, mwaka huu majira ya saa  5:00 usiku wakati marehemu akinywa  pombe hiyo pamoja na watuhumiwa hao nyumbani kwa Jumanne Jailos.

Alisema wakiwa eneo hilo marehemu  aliwaambia wenzake kuwa kofia yake imeibiwa akiwa hapo ndipo watu hao walipowahisi watoto  wa Jumanne waliokuwa wakiwauzia pombe hiyo kuichukua, hivyo kuanza kuwachapa viboko lakini kofia hiyo haikuweza kupatikana.
Kamanda Nley  alisema  baadaye watuhumiwa  hao waliamua kumpekua marehemu ili kutaka kupata ukweli kwamba kofia hiyo anayo au la, na baadaye kuikuta ikiwa ndani ya suruali yake na walipomuuliza aliwajibu kuwa alikuwa amesahau kama alikuwa ameiweka mfukoni mwake.

Baada ya kuona hivyo watuhumiwa  hao walitaka marehemu naye  aadhibiwe  kwa kuchapwa viboko  kwa kuwa aliwasababishia watoto  hao kuchapwa viboko kwa kosa ambalo  halikuwa lao.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, wakati watuhumiwa hao wakimchapa marehemu viboko visivyo na idadi aliamua kujihami kwa kuchukua kigoda  na kuwarushia, hali iliyosababisha amjeruhi Jumanne.

Alisema tukio hilo liliwafanya wapate hasira ndipo nao walimshambulia marehemu kwa mateke na ngumi, hali iliyomfanya apate maumivu kisha aliondoka na kurudi nyumbani kwake na siku iliyofuata alifariki dunia akiwa nyumbani hapo majira ya mchana.
Kamanda Nley  alisema watuhumiwa  watafikishwa mahakamani wakati wowote  upelelezi utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment