Pages

Tuesday, May 7, 2013

CHADEMA yamsaidia mtoto matibabu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemkabidhi hundi ya sh milioni 1.3, Celina Peter, mama wa mtoto Beatrice Shemtibuka, anayesumbuliwa na matatizo ya moyo anayetakiwa kupelekwa India kwa matibabu.

Hundi hiyo alikabidhiwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha, Maltin Sarungi, ikiwa ni mchango wa wanachama na wapenzi wa chama hicho kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.

Sarungi alisema fedha hizo zilichangwa na wanachama kupitia mkutano wa hadhara baada ya mama huyo kumueleza Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, matatizo yanayomkabili mwanae.

Alifafanua kuwa mbunge akalazimika kulizungumzia suala hilo katika mkutano huo na kuwaomba wanachama na wapenzi kumsaidia mama huyo ambapo yeye kama mbunge aliahidi kusaidia tiketi ya kwenda India kwa matibabu ya mtoto huyo.

Akizungumzia chanzo cha tatizo la mtoto wake, mama huyo alisema awali alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kukosa sehemu ya haja kubwa na kulazimika kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baada ya tatizo hilo kwisha akabainika ana tatizo la moyo.
 “Lions Club wameahidi kunisaidia dola 2,000, hivyo nilikuwa natafuta dola 2,700 zilizobaki ambapo nashukuru kupata msaada huu kutoka CHADEMA na mbunge kuniahidi tiketi za kwenda India,’’ alisema Selina.
Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha, Effata Nanyaro, alitoa wito kwa serikali kujitahidi kuboresha sekta ya afya nchini ili kuwezesha wenye matatizo kama hayo waweze kutibiwa hapa nchini.

No comments:

Post a Comment