Pages

Sunday, May 12, 2013

CRDB yawafunda wanawake wajasiriamali.

WAJASIRIAMALI wanawake nchini wametakiwa kutumia vema fursa zenye tija zilizopo katika Akaunti ya Malkia ya Benki ya CRDB ili kuharakisha harakati za maendeleo yao kibiashara na kijamii.

Hayo yalisemwa na Ofisa Masoko Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo akiwasilisha mada katika kongamano la wanawake lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, likihusisha wajasiriamali wanawake.

Kiondo alisema kuwa harakati za maendeleo kwa mwanamke ni muhimu kwa ustawi wa taifa na jamii na Malkia ya CRDB, ni njia sahihi itakayomuwezesha mjasiriamali huyo kuokoa pato lake ambalo awali lilikabiliwa na changamoto nyingi.
“Malkia Akaunti ni mkombozi wa kweli wa mjasiriamali mwanamke, ikibeba tija nyingi na kumuepushia adha zilizopo katika aina nyingine ya uwekezaji. Akaunti hii inatoa mkopo wa dharura wakati wa matatizo, wa asilimia 80 ya akiba yako, bila kuathiri chochote,” alisema Kiondo.

Aliwakumbusha wanawake kuhakikisha wanaepuka kero na changamoto zinazohatarisha harakati zao, kwa kuwekeza pesa zao kupitia akaunti hiyo, ambayo imewanufaisha wengi miongoni mwa wanawake wenye malengo tofauti.
Kongamano hilo la wanawake lilifanyika chini ya udhamini wa CRDB kupitia akaunti ya Malkia.
Wakizungumzia kongamano hilo, baadhi ya washiriki walipongeza mada na ushuhuda uliotolewa na waelimishaji, ambao umewaongezea hamasa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kibiashara na kupanua wigo wa maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment