Pages

Sunday, May 5, 2013

‘Msiwape wajawazito dawa hovyo’.

MBUNGE wa Viti Maalumu, Felister Bura (CCM), amewataka wakazi wa Dodoma kuacha kuwapa wajawazito dawa ambazo hazijathibitishwa na wataalamu wa afya ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Bura aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za maendeleo za kata za Hombolo, Viwandani na Madukani.
Mkutano huo ulilenga katika kuhamasisha shughuli za mradi wa Tuunganishe Mikono (JHI) unaoendeshwa na taasisi ya Aga Khan kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, chini ya ufadhili wa Shirika la kimataifa la Maendeleo la Canada (CIDA).

“Watu wa Mpunguzi hawapo hapa, lakini kuna hili jambo la watu kuwapa dawa za kienyeji wanawake wajawazito ili wajifungue mapema halafu wanakuja kupata matatizo,” alisema.
Pia aliwataka wakazi hao kuhakikisha wanawapeleka mapema wajawazito hospitali ili waweze kupata uangalizi wa wataalamu na kuepusha vifo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Dk. Festo Mapunda, alisema mradi huo unalenga katika kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto.

“Takwimu zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito katika Wilaya ya Dodoma ni 97 kati ya wajawazito 100, 000 na kwa upande wa watoto vifo ni 16 kila vizazi hai 1,000,” alisema.
Alisema mkakati wa Mkoa wa Dodoma ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga walio chini ya umri wa miaka mitano.

No comments:

Post a Comment