Pages

Thursday, May 30, 2013

Sofapaka kuwapima wapya wa Yanga, Simba

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Sofapaka ya Kenya, inatarajia kuwasili nchini Juni 10, kwa ajili ya kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Yanga na Simba.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Smartsports, George Wakuganda, amesema kuwa, mechi hizo zitakuwa nzuri kwa timu zote kuwajaribu wachezaji wapya.

“Hii itakuwa nafasi nzuri kwa timu zote kuwajaribu wachezaji wao wapya watakao wasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara,” amesema.

Wakuganda amesema baada ya Sofapaka kuwasili jijini Dar es Salaam, itacheza mechi yake ya kwanza Juni 12 dhidi ya Simba, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Sofapaka wataanza kucheza na Simba Juni 12, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, tunaamini Wekundu wa Msimbazi watatumia nafasi hii kuwaonesha mashabiki wao vifaa vyao vipya,” amesema.

Mkurugenzi huyo wa Smartsports, alisema Juni 13, kikosi hicho kutoka Kenya kitashuka tena uwanjani kuumana na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Afrika Mashariki (Kombe la Kagame), Yanga.

Amesema mechi hiyo itakuwa nafasi nzuri kwa mashabiki wa timu hiyo kuwaona wachezaji wao wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao, Mrisho Ngassa na wengine, wakiwa wamevaa jezi za rangi ya njano na kijani.

Yanga hivi karibuni imewatangaza wachezaji wapya wawili, wakitokea Simba, huku Haruna Niyonzima akiongeza mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo.

No comments:

Post a Comment