Pages

Monday, May 13, 2013

Wabunge wailipua mifuko ya jamii.

WABUNGE wameichachamalia mifuko ya hifadhi za jamii wakidai inakusanya fedha nyingi kwa wanachama, lakini huduma zake hazikidhi mahitaji na matarajio ya wahusika.

Hali hiyo ilijitokeza jana wakati wa semina kwa wabunge iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ikiwa ni ya pili kwa ajili ya kuwapa uelewa wabunge kuhusu huduma za mifuko hiyo.
Katika michango yao, baadhi ya wabunge walielekeza malalamiko yao mengi kwa Mfuko wa 

Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakisema kuwa unawalenga zaidi matajiri.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy (CCM), ndiye alikuwa wa kwanza kuishambulia NSSF akisema kuwa inakopesha matajiri ambao hata wakati mwingine wanashindwa kulipa madeni hayo.

“Hii mifuko mikubwa ya NSSF, PPF na wengine wanajenga vijumba vya hovyo vyenye vyumba viwili halafu wanawauzia wanachama kwa sh milioni 70. Huu ni wizi, hakuna nyumba ya vyumba viwili inaweza kuuzwa kwa kiasi hicho,” alisema.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliipa changamoto mifuko hiyo kufikiria zaidi kwenye uwekezaji wa miradi ya kukuza uchumi kama vile reli na umeme.

“Uwekezaji wa mifuko hii kila wakati ni kwenye majengo ambayo kitaalamu hayakuzi uchumi, kwanini wasifikirie kujielekeza kwenye reli na umeme,” alihoji.
Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (CHADEMA), alidai kuwa NSSF inawaibia wanachama kupitia nyumba inazowauzia.

“Mimi nimeuziwa nyumba kule Kijichi jijini Dar es Salaam kwa sh milioni 103 halafu kila mwaka nakatwa sh 1.2 ambayo itakatwa baada ya miaka 20, hiyo ni nyumba ya aina gani inaweza kulipiwa fedha kiasi kikubwa hivyo?” alihoji.

Pia alihoji kuponi kwa ajili ya wanachama wa NSSF ambao wanatakiwa kupata huduma za matibabu mbali na hospitali wazozichagua ili kuwaondolea usumbufu.
Susan Kiwanga wa Viti Maalumu (CHADEMA) naye alihoji ni kwanini NSSF iwalazimishe wanachama wake kukopa kupitia Saccos ilhali wakati wa kujiunga hawapewi utaratibu huo.

Alizungumzia masharti ya fao la kujitoa yanayomtaka mwanachama awe amefikisha miaka 60 akisema ni kuwatesa wategemezi kwani umri wa kuishi Mtanzania ni miaka 47 na kwamba kwa masharti hayo mwanachama atakuwa amekufa.
Mfuko mwingine ambao ulilalamikiwa na wabunge ni ule wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF), wakisema kuwa dawa hazipatikani katika hospitali na kwamba pia zinauzwa kwa bei kubwa ambayo ni mara mbili zaidi ya ile halali.

Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM), Ally Keisy (CCM) na Said Arfi wa Mpanda Mjini (CHADEMA), walitaka ufanyike utaratibu wa kuwawezesha wananchi wote kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.
Mifuko hiyo ambayo inasimamiwa na SSRA ni NSSF, PPF, PSPF, LAPF, GEPF na NHIF ambayo jana wakuu wake walipata nafasi ya kueleza huduma zao kwa wabunge.

Akijibu hoja za wabunge, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka alisema kuwa bado mchakato wa kuhusu fao la kujitoa kwa wanachama unaendelea kufanyiwa kazi pamoja na suala la pensheni ya pamoja kwa mifuko yote.
Kuhusu nyumba zinazojengwa na mifuko hiyo kuuzwa kwa bei kubwa, Isaka alisema ni kutokana na utaratibu wa kutumia zabuni wakati wa ujenzi, lakini aliongeza kuwa baadaye watakuja na mwongozo mbadala ili kutoa unafuu ambao mwanachama ataweza kukopeshwa kiwanja ajenge mwenyewe.

No comments:

Post a Comment