Pages

Friday, May 10, 2013

Wanawake msitumiwe na wana siasa - Kairuki

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, amewataka wanawake nchini wasiwe ngazi ya wanasiasa kufanikisha mambo yao bali watumie wingi wao katika kuhakikisha agenda za kuwakomboa zinafanimkiwa.

Kairuki alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua Ilani ya wanawake wa Tanzania katika Katiba mpya, uzinduzi uliofanyika Mabibo jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Alisema ingawa sensa iliyofanyika mwaka jana inaonesha wanawake ni asilimia 51 ya Watanzania wote bado nafasi yao ya kumiliki uchumi wa nchi hailingani na wingi wao huku katika nafasi za uamuzi wakiwa hawafiki katika asilimia hizo.
Kutokana na hali hiyo, Kairuki aliwakumbusha TGNP kuwa kazi iliyo mbele yao kuwakomboa wanawake ni kubwa kuliko mafanikio yaliyopatikana katika miaka yote ya harakati za ukombozi wa mwanamke katika Tanzania.

“Ninyi TGNP mmefanya uamuzi wa makusudi wa kuwaunganisha wanawake nchini kuwa na agenda ya sauti moja bila kujali itikadi na tofauti zao katika kutengeneza Katiba mpya, 

Katiba ya nchi ni nyenzo muhimu sana katika kurekebisha dosari za kihistoria zilizowanyima wanawake fursa sawa katika nchi,” alisema Kairuki.
Alisema umoja wa wanawake katika kupigania haki yao itawafanya waingie katika ngazi za uongozi itawaondolea minyororo ya kutokumiliki mali na itawawekea ulinzi dhidi ya mila na sheria kandamizi dhidi ya ustawi wao.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Ussu Mallya, alisema madai ya wanawake katika Katiba mpya yanatokana na mawazo ya makundi mbali mbali yaliyopata fursa kushiriki semina za kila Jumatano inayoendeshwa na mtandao huo.

No comments:

Post a Comment