Pages

Sunday, May 12, 2013

Watetezi haki za binadamu watoa tamko zito.

MTANDAO wa watetezi wa haki za binadamu nchini wameelekeza tuhuma kwa serikali katika masuala mbalimbali yahusuyo utendaji huku wakiilaumu kuwa imeshindwa kuongoza vema.

Badala yake wamesema serikali imeanza kutishia wanaharakati na waandishi wa habari na hali hiyo imesababisha wananchi kuanza kujichukulia sheria mikononi.

Katika tamko lao la kufunga mafunzo yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, watetezi hao walisema kushamiri kwa vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi, kuteka, kutesa, kung’oa meno, na macho, kukata vidole na hata kuwarushia mabomu waamini wakiwa katika maeneo ya maombi, ni ishara ya serikali iliyoshindwa kutimiza majukumu yake.

Badala yake imewekeza katika matumizi ya nguvu kuwakandamiza watetezi wa haki za binadamu kwa namna mbalimbali, ikiwemo kuwafungulia kesi huku watetezi wakishutumiwa kuwa ni wapinzani kwa sababu kazi zao zimekuwa zikilinganishwa na kazi za vyama vya upinzani na za kiuchochezi.
Watetezi hao wameiasa serikali ielewe kuwa watetezi ni kiungo muhimu katika kuibua na kufichua maovu ili kujenga utawala unaoheshimu haki za binadamu.

Aidha, katika tamko hilo waliongeza kuwa wanahabari wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama huku wamiliki wa vyombo hivyo wakiwa hawana mikakati mizuri ya usalama wa waandishi wao.

“Pia malipo finyu kwa wanahabari ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibiwa kwa habari za kweli kwa sababu baadhi yao hawapati malipo ya uhakika wala mikataba,” lilisema tamko hilo.

Wanaharakati hao pia wameliasa Jeshi la Polisi liwe makini kuepuka matumizi ya silaha za moto na nguvu za ziada ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu wa kudumu.
“Katika purukashani nyingi za kisiasa jeshi hilo limeshindwa kabisa kuonyesha kwamba linafanya kazi ya kuutumia umma wa Watanzania wote na badala yake limekuwa likichukua mwelekeo wa kuwatumikia wanasiasa au chama fulani,” ilisema taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment