Pages

Sunday, June 23, 2013

CCM wajipanga kuinusuru bajeti

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kiko kwenye mkakati kabambe wa kuhakikisha Bunge linapitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Kesho Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wanatarajiwa kuhitimisha kujibu hoja za wabunge kisha Bunge kupiga kura za kuipitisha.

Kwa mara ya kwanza, katika historia ya vyama vingi, bajeti ya serikali haikujadiliwa na wabunge wa kambi rasmi ya upinzani ya CHADEMA kutokana na kutokuwapo bungni kwa wiki nzima.
CHADEMA ambao walihamia jijini Arusha kwa ajili ya mazishi na maombolezo ya wafuasi wao waliouawa kwenye mlipuko wa bomu Jumamosi iliyopita, waligoma kuwasilisha hata bajeti yao mbadala bungeni.

Hatua ya kutowasilisha mezani hati ya msemaji mkuu wa kambi hiyo kwa Wizara ya Fedha, Kabwe Zitto, kwa mujibu wa kanuni za Bunge inamaanisha kuwa hotuba yao hiyo haikuingizwa kwenye rekodi rasmi za Bunge ‘hansard’.

Ijumaa wiki hii, Spika wa Bunge alitangaza kufunga mjadala wa wachangiaji wa bajeti hiyo, akisema kuwa wabunge waliokuwa wameomba kuchangia wote walipata nafasi isipokuwa wale walioomba lakini wakapata dharura.

Kwa mantiki hiyo, CHADEMA ni kwamba hawakushiriki kwa lolote katika bajeti kuu ya serikali, iwe kwa kupitia maoni ya kambi au mchango wa mbunge mmoja mmoja.
Kutokuwapo kwa CHADEMA wiki nzima, kumeleta mdororo bungeni kutokana na mjadala kuegemea upande mmoja wa wabunge wa CCM, japo wabunge wote watano wa NCCR-Mageuzi na wachache wa CUF walijitahidi kutoa michango ya kusisimua.

Wabunge machachali wa CCM, Deo Filikunjombe wa Ludewa, Kangi Lugola wa Mwibara nao hawajaonekana bungeni zaidi ya wiki na vile vile Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Ali Keissy wa Nkasi Kaskazini wamepinga bajeti hiyo.
Hali hiyo ni kama imemtisha Spika wa Bunge, Anne Makinda na kuanza kutilia shaka kuwa huenda bajeti hiyo ikakwama kupitishwa kutokana na idadi ya wabunge kutotimia.

Akiahirisha Bunge juzi, Spika aliwataka wabunge wote kuhakikisha wanahudhuria Bunge kesho, huku akiwahimiza mawaziri walioko safarini au wale wanaokusudia kusafiri wasitishe safari hizo hadi bajeti hiyo itakapokuwa imepitishwa.
Hatua ya CHADEMA kutoshiriki mjadala wa bajeti, bado inatia hofu kama wabunge hao kesho wataingia bungeni wakati wa kuipitisha bajeti hiyo.

Katika maelekezo yake juzi, Spika Makinda alilazimika kuwasomea wabunge kanuni kuhusu nini kitatokea endapo bajeti hiyo kuu ya serikali itashindwa kupita.
Bila kufafanua vizuri kusudio lake, Makinda alisema anawakumbusha tu ili wafahamu kuwa idadi yao isipotimia bajeti hiyo haiwezi kupita na kwamba hali hiyo ikitokea  mara tatu Rais atalivunja Bunge.

Alisema utaratibu unaotumika kwenye kupitisha bajeti za wizara ni tofauti na ule wa bajeti kuu kwani wakati wa kupiga kura kila mbunge anaitwa kwa jina kisha anasema kama anaiunga mkono au anaikataa.
CCM katika kuhakikisha bajeti hiyo inapitishwa, wabunge wake wengi wamekuwa wakiipigia debe na kuwashawishi wenzao waiunge mkono ili fedha zilizoidhinishwa kwa wizara ziweze kutolewa haraka.

Katika kuwekana sawa, Katibu wa wabunge wa CCM, Jenista Mhagama, aliitisha kikao cha wabunge hao jana saa tano katika ukumbi wa Msekwa mjini hapa.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kikao hicho ni kwa ajili ya wabunge hao kujipanga kuiunga mkono bajeti hiyo ili ipitishwe na idadi inayotakiwa hata kama wabunge wa upinzani na wale wachache wa CCM wasipoiunga mkono. 
Via Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment