Pages

Saturday, June 1, 2013

Kesi yaiweka pabaya TFF

KESI iliyofunguliwa mkoani Pwani dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeonekana kuliweka pabaya shirikisho hilo, ambalo hivi sasa linahaha ifutwe.

TFF imeburuzwa mahakamani mjini Kibaha na mdau wa soka, anayejulikana kama Babu Adam ambaye alifungua kesi Mei 30 mwaka huu, na kusimamiwa na Daniel Ngasa wakitaka haki dhidi ya Kiluvya United, iliyopokwa ubingwa wa mkoa wa Pwani.
Kamati hiyo, iliamua kuivua ubingwa Kiluvya United, baada ya kupokea malalamiko kutoka timu ya Al Etihad ya Mafia, ambayo ilikuwa mshindi wa pili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni, alisema wamekitaka Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (Corefa), kifute kesi hiyo kwa manufaa ya soka la Tanzania.
Kayuni ambaye pia ni Mkutugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo, alisema, tayari amekiandikia barua chama hicho, kukiagiza kishirikiane na mdau huyo kufuta kesi hiyo kabla ya saa 11 jioni ya jana ili kuondoa uvunjwaji na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za katiba ya Corefa na TFF.

Alisema kuwa ibara ya 13 kipengele cha 14 katika Katiba ya Corefa, hakiruhusu kupeleka suala lolote la soka mahakamani kama ilivyo katika Katiba ya TFF, jambo ambalo kama Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), litabaini kuwepo kwa hali hiyo, Tanzania inaweza kufungiwa.
“Kama mnavyofahamu, timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iko safarini kwa ajili ya mchezo wa kimataifa na Morocco, sasa siwezi kuingilia uhuru wa mahakama, kwa kuwa kesi iko mahakamani, ila kupitia Corefa, kesi hii ifutwe mara moja kwa kuwa Fifa wakisikia kuwa tumekwenda kinyume na katiba, watairudisha timu yetu na haitashiriki mashindano yoyote,” alisema Kayuni.

Alibainisha kuwa Corefa wanao wajibu kuhakikisha wanaweka mambo sawa haraka iwezekanavyo, kabla hayajaathiri mfumo mzima wa TFF, kutokana na katiba zenyewe kutoruhusu masuala ya soka kupelekwa mahakamani.
“Mimi mwenyewe ndiyo nilikwenda kuisikiliza kesi hiyo jana mjini Kibaha, lakini siwezi kuizungumzia sana ila ikiwa Corefa hawatafuta kesi hiyo leo, basi Kamati ya Ligi itakutana kesho ili kutoa msimamo wake,” alisema Kayuni.

No comments:

Post a Comment