Pages

Monday, June 24, 2013

Rais Dk. Jakaya Kikwete amesema Viongozi wa dini himizeni amani na utulivu nchini.

Rais Dk. Jakaya Kikwete amesema viongozi wa dini ndiyo wanaoweza kuwaongoza waumini wao katika maisha ya amani na utulivu.

Amesema serikali inategemea mchango wao katika kuidumisha nchi katika hali hiyo.
Dk Kikwete alisema hayo mjini hapa baada ya maadhimisho ya ibada ya misa takatifu ya Jubilee ya miaka 25 ya Mhashamu Askofu Telesphori Mkude wa jimbo Katoliki la Morogoro.

Maadhimisho yalifanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya St Peter na kuhudhuriwa na maaskofu wa majimbo yote Tanzania bara na visiwani, waumini na wageni.

Aliwataka viongozi wa Kanisa Katoliki kuendelea kuwalea vijana katika maadili mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu na kudumisha amani, utulivu, upendo na mshikamano ili taifa lisiangamie.

Alimpongeza Askofu Mkude kwa jitihada mbalimbali anazofanya katika kuboresha huduma za afya na elimu katika jimbo hilo hali inayosaidia jitihada za serikali za kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Serikali inatambua mchango unaofanywa na kanisa Katoliki katika kuleta maendeleo ya nchi hasa katika kuchangia huduma mbalimbali za kijamii, kama elimu na afya na Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizo,” alisema Dk. Kikwete.

Naye Askofu Mkude akishukuru alisema kuwa gharama ya wito ni uaminifu na uadilifu ndani na nje ya kanisa na hata walioko katika ndoa, na wengine waliopewa dhamana mbalimbali katika maisha ya binadamu wanapaswa kuzingatia misingi hiyo.

Alisema kwa miaka mingi kuanzia familia zao, wao wenyewe na vizazi kwa vizazi wamekuwa wakichanganyika Wakristu kwa Waislam bila kujali matabaka ya kiimani, hivyo inashangaza kuona kwa siku za karibuni fujo na mambo mengine yenye itikadi za kiimani kama kuchinja yameanza kusababisha ugomvi.

“Mbona hatugombaniani makaburi wala kuzika? kuna nini kwenye kuchinja kuna malipo fulani mbona toka zamani tulikuwa tunafanya na hatukufika huko, siyo sahihi kwa mkuu wa mkoa wala wa wilaya kubainisha nani ana haki ya kuchinja, hilo sio jukumu lake, kwani haliko kwenye katiba ya nchi, mipaka inafaa kujulikana na tukielekezana hatugombani,” alisisitiza Askofu Mkude.

Askofu Mkude alitoa wito kwa Serikali kuwadhibiti watu kutoka nchi nyingine ambao wanaonekana kufika nchini na kusababisha baadhi ya vurugu zinazojitokeza.

Awali kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Cardinali, Polycarp Pengo, alisema mara nyingi binadamu wamekuwa wakijisahau pindi wanapokumbana na matusi na dharau na kumuweka Yesu pembeni na kuanza kuhangaika, mambo ambayo hayapaswi kufanywa na Mkristo wa kweli.

Alisema ili wafanikiwe safari yao ya kiroho na kimaisha ni vyema wakamtanguliza Mungu kwa kila jambo.
Alisema kuwa nafasi ya jubilee kwa Mkristo ni wakati wa kudhihirisha imani na kumwomba Mungu radhi kwa yale yaliyowateteresha kipindi cha nyuma na kuanza maisha mapya yaliotukuka.

Naye Msaidizi wa Askofu jimbo Katoliki la Morogoro Padre, Patric Kung’alo alisema kuwa umoja wa mapadri jimbo la Morogoro umechanga kiasi cha Sh. 7,890,000 kwa ajili ya kuzindua mfuko wa bima ya afya wa AAR wa Nairobi nchini Kenya utakaotumika kutoa matibabu kwa Askofu wa jimbo Katoliki la Morogoro Telesphori Mkude.
Fr Kung’alo alisema kuwa mfuko huo pia utatumika kwa malipo ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kwa kadi ya kijani kwa mapadri 25 wa jimbo hilo na kwamba waumini wa jimbo hilo wamempatia askofu Mkude zawadi ya Shilingi milioni 25 pamoja na magurudumu matano ya gari yaliotolewa na umoja huo wa mapadri.

No comments:

Post a Comment