Pages

Tuesday, June 25, 2013

Ukipewa pendo la kweli usilipe maudhi.


NAAM kama kawaida tumekutana tena kwenye safu yetu ya Mapenzi na Uhusiano kama ilivyo ada ili kumbushana mawili matatu yahusuyo mahaba hasa yale yanayokwaza na kuondoa maana halisi ya mapenzi.

Napenda kutoa pole nyingi kwa familia ya aliyekuwa mchezaji wa zamani Abdallah Msamba na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Langa Kileo ambao waliwapoteza ndugu zao hao wiki iliyopita. Inaonekana upepo mbaya umekuwa ukivuma kwa sasa, lakini wote tuamini hili nalo litapita, la muhimu kuwaombea marehemu wote wapumzike kwa amani. Baada ya kusema hayo, tuendelea na mada yetu ya leo, wote tunajua mapenzi yanajumlisha upendo wa pande mbili kati ya mwanamke na mwanaume wala hakuna aliyeumbwa kwa ajili ya kupendwa au kupenda vitu hivyo havipo. 

Maana halisi ya mapenzi ni kupendana, siyo dhambi kumuonyesha mwenzio unavyo mpenda au mwenzio kuonyesha anavyokupenda. Hii ndiyo sababu ya kuwa wawili lazima mjiulize kuna wanaume na wanawake wangapi lakini amekuchagua wewe! Upendo wa dhati dunia ya leo imekuwa adimu kama maji jangwani, sasa hivi mapenzi yamekuwa shaghalabaghala  yamebakia mapenzi ya mtu kitu, asiye na kitu hajui mapenzi au kwa wenye umbile na sura nzuri, wenzangu na mimi tulie tu.

Tumeona wengi wakilia baada kupanda mbegu ya mapenzi pasipo na mapenzi, lakini walio bahatika kupata wenye mapenzi ya kweli wamesahau nini maana ya mapenzi na kujikuta wameyageuza badala ya kuwa furaha yanakuwa mateso kwa wenzao kwa vile wameonyesha kuwa wanapendwa. Siku zote anayependa ndiye anayeteseka kwa kujitahidi kuonyesha upendo wake ambao hauthaminiwi.

Mateso huja pale anapoamini kuna kitu anakosea katika penzi lenu bila kujua aliyempa penzi lake hajui thamani yake.  Penzi linakuwa na masharti kibao kwa kujua huwezi kukataa kwa vile unampenda au linakuwa la gharama kwa kutaka vitu vya thamani ambavyo wakati mwingine vinakuwa nje ya uwezo wako. Jua kuwa ni kosa kumfanya mpenzi wako ajute kuwa na wewe, siku zote penzi tamu ni kwa mpenzi wako kukuona kama tulizo la moyo wake, kato la uchovu wa kutwa nzima.

Mfanye mpenzi wako akiwa mbali nawe akuwaze au ukikumbuka, atabasamu na kuwa na hamu ya kukuona.  Kila akikukumbuka au akisikia jina lako likitajwa atamani muda ufike upesi ili awe pamoja nawe. Siyo kila akisikia jina lako au kila akikukumbuka moyo wake unamlipuka na kujuta kwa nini alikupenda au amekaa na wewe. Heshimu na kuthamini upendo unaopewa na mpenzi wako, kama mwenzako kaonyesha anakupenda jua una deni la kulipa upendo huo.

Usiwe mwizi wa fadhila kupewa pendo kulipa maudhi mpende akupendaye. Mwisho narudia kwa kusema kumbuka karaha katika mapenzi humtia mtu sugu katika moyo wake na kufikia kukuchukia na kukuona adui wa moyo wake. Ipo siku mapenzi hutoweka na kukuona adui yake namba moja kuliko kifo.
 
Aliyekuwa akikupenda siku akikuchukia huwa hana msamaha atakufukuza kama mbwa na kushangaa, kisha atajiuliza ni kweli ni yeye ndiye uliyekuwa ukimpeleka puta kama saa mbovu! Upendwapo, pendeka utakuja penda pasipo penzi utatamani ardhi ikumeze

No comments:

Post a Comment