Pages

Monday, June 24, 2013

Wasanii wa filamu Iringa waunda shirikisho.

WASANII wa filamu mkoani hapa, wametakiwa kufanya kazi zao kwa ushirikiano na kuaminiana ili zipate kujulikana kitaifa na kimataifa, hivyo kujiongezea kipato.
 
Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa Muda wa Shirikisho la Filamu Mkoa wa Iringa, 
Daudi Masasi, kwenye kikao cha kuandaa rasimu ya katiba ya shirikisho hilo ambapo wasanii wa filamu mkoani hapa walikutana kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa.

Masasi aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa gazeti la Tabasamu na mtunzi mahiri wa hadithi, alisema Mkoa wa Iringa una wasanii wengi wenye vipaji ila kutokana na kutokuwa na umoja na kutojiamini, wameshindwa kujulikana kitaifa hadi wakimbilie jijini Dar es Salaam.
 
“Kutokana na kukosa ushirikiano, kujiamini na uaminifu unaosababishwa na ujuaji wa wasanii wa hapa, ndiyo maana tunashindwa kufanikiwa na kujulikana licha ya wengi kutoa filamu na kushindwa kufanya vizuri katika soko,” alisema Masasi.

Aliongeza kuwa lengo la kuanzisha Shirikisho la Wacheza Filamu Mkoa wa Iringa ni kuleta umoja ili kazi zao zijulikane na kupendwa na watazamaji na kujiongezea kipato.
Aidha, alisema lengo la shirikisho ni kuwatetea wasanii haki zao na kupata maslahi wakati wa uchezaji wa filamu kutokana na wengi wao kutolipwa malipo mara baada ya kucheza filamu husika.

 Naye Katibu wa Muda wa Shirikisho hilo, Shabani Mwinyikayoka alisema umoja ni kitu muhimu katika kukuza tasnia hiyo mkoani hapa, hivyo ni muhimu wasanii wajikite kwenye ubora wa kazi.

Aliongeza kuwa wasanii wa Mkoa wa Iringa wameshindwa kupiga hatua kutokana na ubinafsi, hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
 Alitaja changamoto nyingine ni kukosekana kwa elimu miongoni mwao, ikiwemo ile ya darasani, hivyo kushindwa kupata mafanikio katika kazi hiyo.
 
“Nimeanza kazi ya sanaa tangu mdogo, hivyo najua ni kiasi gani wasanii wasivyokuwa na upeo wa sanaa hii, na kama huna la kusema acha kusema na ukisema utasema lisilo la maana. Wasanii twendeni shule kuweza kuwa na upeo wa sanaa hii,” alisema Mwinyikayoka.

Aliwaomba wasanii zaidi ya 80 waliojitokeza katika mkutano  wao kuishi maisha ya nidhamu, heshima kama wanavyoigiza kutokana na jamii kuiamini sana kazi ya sanaa.
 Aidha, alisema shirikisho litakuwa na mikutano ya mara kwa mara na kuanzisha bonanza la kila wiki na kufanyika kila Jumamosi katika Uwanja wa Samora lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kujenga upendo miongoni mwa wasanii.
Mlezi wa shirikisho hilo, Fedrick Mwakalebela aliahidi kutoa vifaa vya michezo kwa shirikisho hilo ikiwemo mipira ya soka, mipira wa mikono, jezi na msaada wa fedha katika usajili wa shirikisho hilo.

Alisema sanaa ya filamu mkoani hapa iko chini sana, hivyo ni jukumu la wadau wote kuwasaidia wasanii mkoani hapa na kuzalisha ajira kwa njia ya filamu.
 “Nitajitolea vifaa vyote vinavyohitajika, na nitakuwa mlezi wao katika kuwatafutia masoko ndani na nje ya Tanzania. Kwa kuanza nitatoa vifaa vya michezo,” alisema Mwakalebela. 

No comments:

Post a Comment