Pages

Wednesday, July 24, 2013

Exim yaahidi kuendeleza ukuzaji uchumi.

Dar es Salaam. 
Benki ya Exim Tanzania imesema itaendelea kusaidia jitihada mbalimbali za kusaidia ukuaji uchumi nchini, ili kuhakishisha wananchi wananufaika.
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Exim, Yogesh Manek (katikati) akizungumza kwenye uzinduzi wa jarida la benki hiyo lijulikanalo kama ‘Eximite’ litakalokuwa likitoka kila robo ya mwaka. Kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu, Dinesh Arora na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Anthony Grant.

Akizungumza kwenye  uzinduzi wa Jarida la Eximite juzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Exim, Yogesh Manek, alisema ripoti mbalimbali zimeonyesha nchi nyingi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania zinaendelea kupata maendeleo kwa kasi. Manek alisema ripoti inaonyesha sekta ya benki ina kazi ya kuhakikisha upatikanaji fedha haraka, ili kufadhili miradi ya uwekezaji.
“Ripoti zinaonyesha nchi za Afrika Mashariki zinakaribisha zaidi uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI). Benki zinatakiwa kutoa mchango mkubwa wa  fedha kwa miradi hiyo,” alisema Manek na kuongeza:

“Exim itaendelea kutoa mchango wake kusaidia shughuli mbalimbali za uwekezaji pindi zitakapo jitokeza. Malengo yetu sasa ni kuhakikisha benki inatoa huduma za pekee zitakazosaidia fursa za uwekezaji zitakazojitokeza miaka ijayo.” 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Anthony Grant, alisema wataendelea kutekeleza mpango wake wa kutanua huduma zake. Grant alisema wanalenga kufikisha huduma karibu na  na jamii na kusisitiza kuwa benki inatarajia kufungua matawi mengine mawili  mwaka huu. 

“Tumejipanga ndani ya wiki chache zijazo kufungua tawi la kisasa Arusha na kabla ya mwisho wa mwaka  tawi lingine mkoani Tabora,  ni mwendelezo wa mkakati  wa kufikisha huduma karibu na wananchi,”  alisema Grant.

Pia, Meneja Mafunzo na Maendeleo, Priti Punatar, alisema jarida hilo ni uwanja mzuri kwa wafanyakazi kupata nafasi ya kujadili na kusherekea mafanikio mbalimbali ya kikazi na binafsi. Punatar alisema benki imejizatiti kuwa na mfumo bora wa mawasiliano na inatambua umuhimu wa kuwapatia wafanyakazi na wadau taarifa mbalimbali za matukio kuhusu benki hiyo.

No comments:

Post a Comment