Pages

Saturday, August 24, 2013

Kesi ya mchungaji aliyelawiti yaibua utata.

Na Dixon Busagaga, Moshi
KESI ya kutorosha wanafunzi wawili, inayomkabili Jean Felix Bamana, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeahirishwa kutokana na mashahidi wa upande wa Mashtaka kushindwa kufika mahakamani.

Mwendesha mashtaka wakili wa Serikali Abdalah Chavula, aliiambia mahakama kuwa shahidi wa sita katika kesi hiyo Koplo Mfume, mwenye namba AE2524 wa kituo cha polisi Bomang’ombe wilayani Hai, ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuwa na majukumu mengine.

Chavula aliiambia mahakama shahidi wa saba katika kesi hiyo Media Juma kutoka Dar es Salaam alijulishwa kuhusu kuhitajika kutoa ushahidi mahakamani hapo kwa njia ya simu, lakini hadi mahakama inaanza kusikiliza kesi hiyo jana, hakukuwa na mawasiliano yoyote kati yake na shahidi huyo na kwamba shahidi wa nane, Sajenti Mwajuma, alipata dharura ya kikazi.

Hata hivyo, mshtakiwa kupitia kwa wakili wake, Erick Gabriel, alionyesha kutoridhika na maamuzi ya kuahirishwa kwa kesi hiyo kutokana na madai ya mashahidi kutofika mahakamani huku akiwasilisha pingamizi la kukosekana kwa shahidi namba nane, Sajenti Mwajuma ambaye alifika mahakamani hapo na kutoweka muda mfupi kabla mahakama haijaanza.

Wakili Gabriel aliiambia mahakama hiyo kuwa madai kwamba Sajenti Mwajuma alishindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kupata dharura za kikazi ni kuipotosha mahakama kwani shahidi huyo alionekana nje ya mahakama muda mfupi kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

“Mheshimiwa hakimu, naomba kuwasilisha pingamizi katika kile kinachodaiwa kuwa ni kushindwa kufika kwa sajenti Mwajuma, tunaomba kuieleza mahakama yako tukufu kuwa shahidi huyo alionekana muda mfupi katika eneo la mahakama kabla ya kesi kuanza, hivyo hatuelewi ni kwa nini upande wa jamhuri umeshindwa kuhakikisha anafika na kutoa ushahidi wake,” alisema Gabriel.

Kutokana na madai hayo mwendesha mashtaka wa serikali, Wakili Chavula, aliiambia mahakama kuwa huenda kuonekana kwa Sajenti katika maeneo ya mahakama ilikuwa ni sehemu ya kumalizia maombi ya ruhusa.

Awali shahidi wa tano katika kesi hiyo Angela Swai (17) aliileza mahakama ya hakimu mkazi Moshi, mbele ya hakimu Naomi Mwerinde namna mshtakiwa alivyomlazimisha kufanya naye mapenzi bila kutumia kondomu.

Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Aprili 13, mwaka huu, inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo ambaye alitajwa mahakamani hapo kuwa ni mchungaji katika kanisa la TAG Mikocheni la Mama Getrude Lwakatare, inadaiwa kuwa mnamo Februari 14, mwaka huu, aliwarubuni wanafunzi wawili, Angel Swai (19) na mwenzake mwenye umri wa miaka 17 jina linahifadhiwa kwa madai ya kuwasomesha nje ya nchi.

Bamana anashtakiwa kwa makosa mawili ya kutorosha wanafunzi, kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Tanzania chini ya sheria namba 6 ya mwaka 2008, ibara ya 4, kifungu cha 5, kifungu kidogo 4 (i) a.

Kesi hiyo itasikilizwa tena Agosti 30 katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi, baada ya upande wa mashtaka kuahidi kuwaleta mashahidi hao mahakamani hapo kutoa ushahidi wao.

No comments:

Post a Comment