Pages

Monday, August 26, 2013

MAKALA: NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI ...02

Na Irene Mwamfupe Ndauka. 
 ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:Nilichukua kama saa moja kutoka kazini hadi kufika nyumbani. Nje nilikuta mfuko wa rambo  mweusi, ndani yake ulionekana kuwa na kitu kwani ulikuwa umetuna sana. Niliinama kuipekenyua ili nijue ndani kulikuwa na nini, nilishangaa kuona ni vipande vya nyama za kuchoma tena vilikuwa na moto.

“Kha! Atakuwa nani ameweka?” nilijiuliza mwenyewe, nikauacha palepale, mimi nikapanda ngazi za kuingia ndani. Mlango ulikuwa wazi hali iliyoashiria kwamba, wenzangu walisharudi. Nilisukuma mlango, nikaingia. Nilikutana na harufu ya pafyumu, nikahisi walikuwa wakijiandaa kutoka.
 ("Kitabu cha Niliyoyaona Mochwari Sitasahau kinapatikana sehemu zote za Tanzania kwa wauza Magazeti ni Tsh 3000/=tu")

“Jamani za leo?” nilisalimia kwa sauti ya juu licha ya kwamba, mlango wao ulikuwa umefungwa, hakuna aliyeniitikia, hilo sikulijali sana kwani niliamini kwa kuwa walikuwa ndani, isingekuwa rahisi wasikie salamu yangu.

Niliingia sebuleni kwangu, kisha nikaenda chumbani, kuna kitu kilinishangaza, nikasimama kwa mshtuko. Nilikuta sehemu nilipoweka kiberiti asubuhi siyo, nilikiacha juu ya meza, nikakikuta juu ya kitanda. Niliacha kioo na kitana juu ya kitanda, lakini nikavikuta kwenye stuli, niliguna!

Nilikishika kioo cha kukiangalia kwa umakini kama kina mabadiliko yoyote, lakini sikuona, nikashika kitana. Nilipokigaua sana pia sikuona kitu cha tofauti, nikaamua kuchania, nikahisi kuguswa na kitu kama nywele ndefu kama za mtu aliyefuga. Nilikiweka kitana juu usawa wa dirishani, nikaona nywelenywele nene, nyeusi, mwili wote ukasisimka.

Ninavyojua mimi, mwanamke mwenye nywele nyingi akichania kitana, ndiyo huacha nywele, sasa mimi nilikuwa na nywele fupi sana zisingeweza kuacha nywele ndefu kwenye kitana.

“Mh! Hapa kuna kinachoendelea,” nilisema moyoni huku nikikaa. Nilishtuka zaidi kuona soksi zikiwa kwenye msumari nyuma ya mlango wakati niliacha chini.

“Huyu ni nani?” niliuliza kwa sauti ya ukali.
Ghafla nikasikia kicheko kutoka chumbani kwa wale wenzangu.
Nilikaa kwenye kochi, nikaanza kuangalia sehemu mbalimbali za mle ndani ambazo niliamini naweza kuona mabadiliko mengine mbali na yale ambayo nilishayaona, lakini sikubahatika.

Nilitoka, nikaenda sebuleni ambako nako nilianza kuangalia kila kona ya sebule. Nilishangaa kuona glasi ya maji ya kunywa ambayo niliitumia asubuhi kisha nikaacha maji yamejaa, ikiwa haina hata tone la maji mbaya zaidi, iliwekwa juu ya kabati ambapo mimi niliiweka kwenye meza ya katikati ya sebule.

“Mh! Hii kali sasa,” nilijikuta nikisema kwa sauti, mara nikasikia kicheko tena kutokea upande wa pili kule kwa wenzangu. Sasa nikaanza kama kuhisi kitu kuhusu watu hao. Ni kwanini kila nilipoongea kwa sauti ndipo na wao waliangua kicheko?
Niliamua kujaribu tena, nikasema kwa sauti:

“Nitakuja kuua mtu, kweli tena.” Nikasikia kicheko tena, safari hii kilidumu kwa muda.
Moyoni nikasema naanza kufanyia kazi uhusiano wa maneno yangu na vicheko vya wale majirani. Nilitoka kurudi chumbani, wakati napita kwenye korido, nilisimama jirani na mlango wao. Walikuwa wakiongea, lakini niliposimama mimi, kukawa kimya ghafla kama hakuna watu.

Nilipozama chumbani, nyuma wakaanza kuongea tena. Sikufunga mlango ili niweze kusikia wanachokiongea, lakini jamani kwa kusema ule ukweli wa Mungu, sikujua walikuwa wakitumia lugha gani katika kuwasiliana hata pale nilipojitahidi kutega masikio kwa umakini wa hali ya juu sana.

Kuna wakati utadhani wanatumia sana neno dotikom, lakini ukisema usikilize zaidi unasikia wakisema sana kotoko au kiburate, wakati mwingine sauti ya kike ilisema kaunto, ya kiume ikarudia hivyohivyo, kaunto.

Nia yangu kubwa ilikuwa kuwaona kwa sura na kufahamu kama ni ngozi nyeusi au nyeupe. Hilo peke yake lingenipa mwanga ni watu wa aina gani naishi nao pale ndani ya nyumba.
Nilisikia mlango wa chumbani kwao ukifunguliwa na mimi nikatoka haraka sana, cha ajabu sikuona mtu akitoka lakini mlangoni kulikuwa na kandambili pea moja tu wakati zilikuwa pea mbili.

Hilo lilimaanisha kwamba, mmoja wao alitoka kwenda chooni, nilichofanya ni kuamua kusimama katikati ya mlango wangu ili huyo aliyekwenda chooni akirudi nimuone. Ni kweli mmoja wao alikwenda chooni kwani nilisikia mlio wa maji.

Nilijiahidi kusimama mlangoni kwangu kumsubiria. Kwa ramani ya nyumba ile ilivyo, asingeweza kutoka chooni bila mimi kumwona hata kama angekuwa anataka kutoka kwenda nje au uani.

Mlio wa maji ulikosa kusikika, nikawa natumbulia macho kule huku moyoni nikisema:
“Leo ndiyo leo, asemaye kesho mwongo, hata afanyaje, hawezi kunichenga hapa hata kidogo,” nilisema moyoni, ingawa wakati huo mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda kwa kasi.

Nilipoanza kuhisi muda unakwenda na hakuna mtu aliyetoka, nikampa dakika tatu kwamba lazima atakuwa anavaa ndiyo maana anachelewa:

“Labda alikuwa anajisaidia haja kubwa, maana wengine huwa wanavua nguo zote, lakini mimi nipo, siendi kokote,” nilisema moyoni nikiwa bado nimesimama mlangoni kwangu.
Baaad ya muda, nikasikia watu wakiongea chumbani kwao, nikashtuka, nilijikuta nikisema:
“Haa!”

Haraka sana nilitupa macho mlangoni kuangalia kandambili, nikazikuta pea mbili, nikashangaa:

“Ina maana amenipita hapahapa au? Haiwezekani, asingeweza kunipita hata kama ingekuwaje?” niliwaza. Nilitoka kuelekea chooni, nikakuta mlango uko wazi, nikachungulia ndani, hakukuwa na mtu, nikanyoosha mikoni, nikarudi ndani.
Nilifikia kwenye kochi sebuleni, nikahema kwa nguvu kwani niliamini nimo ndani ya miujiza mikubwa ya ndani ya nyumba ile.

“Hivi ni kwanini dalali alinidanganya hivi?” nilijiuliza mwenyewe nikiamini kwamba, dalali aliyenipangisha nyumba ile alijua mchezo mzima ila alitaka kupata fedha tu ndiyo maana alinipangisha bila kunipa tahadhari.

Nilitoka sebuleni, nikaenda chumbani, kitandani nikakuta ‘toilet paper’ ikiwa imekatwa sehemu. Mimi niliicha pembeni ya dirisha, lakini ikaonesha kuna mtu aliichukua na kunyofoa kidogo kisha badala ya kuirudishia palepale, yeye aliiacha kitandani.

Mbali na ‘toilet paper’ pia kuna kikopo chenye vijiti vyenye pamba za masikio kilikuwa kwenye stuli jirani na kitanda, lakini kwa muda huo kilikuwa kimeanguka chini halafu vijiti vimebaki kama vitatu tu kwa maana kwamba, aliyeingia kuchukua ‘toilet paper’ ndiyo huyohuyo aliyechota vijiti vya pamba.

Nilianza kuhisi kuwa sikuwa kwenye nyumba salama, lakini kwa uthibitisho upi?

Usikose sehemu ya 03 siku ya jumatano ijayo...

No comments:

Post a Comment