Pages

Tuesday, August 6, 2013

Nyumba za halmashauri zageuzwa gesti.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya imepata hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na kukosa kumbukumbu za vyanzo vyake vya mapato, zikiwamo nyumba inazomiliki kwa zaidi ya miaka 20 bila kuwatambua wapangaji wake kisheria.

Nyumba hizo tatu ambazo ziko katikati ya mji wa Vwawa wilayani hapa kwa sasa zinatumika kama nyumba za biashara ya kupangisha wageni ‘guest house’, baa na ofisi, ambapo moja ni ofisi ya Ushirika wa Umoja wa Wanawake na nyingine ni ya Tanganyika Farmers Association ( TFA).

Hoja ya upotevu huo wa mapato iliibuliwa na Diwani wa Ihanda, Joel Kasebele na baadaye kuungwa mkono na madiwani wengine kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa Halamshauri ya Wilaya ya Mbozi.

Diwani Kasebele alimuuliza Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo ambaye ndiye katibu wa kikao hicho juu ya mustakabali wa nyumba hizo zinazojulikana kwa majina ya TFA, Selfina na MDC (Mbozi District Council) ambazo zinadaiwa kumilikiwa na halmashauri hiyo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980 ulipoanzishwa mfumo wa serikali za mitaa.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Levison Chilewa, alikiri kuwapo kwa nyumba hizo pamoja na nyingine zilizokuwa zikimilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na baadaye kuiuzia halmashauri hiyo.

Pia alikiri kuwapo kwa wapangaji, lakini haijulikani walikodishwa na nani na ni kwa kipindi gani (miaka mingapi) hadi sasa.

hata hivyo, alijitetea kuwa yeye na wataalamu wengi wa halmashauri hiyo ni wageni, hivyo hawakukuta kumbukumbu zozote ofisini kutoka kwa waliowarithi.
Kutokana na hali hiyo, aliliomba baraza hilo kumpatia muda kulifuatilia jambo hilo na kuahidi kulitolea maelezo katika kikao kijacho.

Habari na na Kenneth Ngelesi, Mbozi ,Tanzania daima.

No comments:

Post a Comment