Pages

Thursday, August 1, 2013

Polisi wa Oysterbay kortini wakituhumiwa kwa ujangili.

Kibaha. 
Polisi wawili wa Kituo cha Oysterbay Dar es Salaam na raia wengine saba, wanaotuhumiwa kukutwa wakisafirisha meno 70 ya tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh850 milioni, wilayani Kisarawe wamefikishwa mahakamani.
 
Washtakiwa walifikishwa Mahakama ya Mkoa wa Pwani jana, huku polisi hao wakiwa tayari wamefukuzwa kazi mapema asubuhi hiyo jana.

Wakili wa Serikali, Cesilia Shelly, alidai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanashtakiwa kuhusika na makosa mawili; Kukutwa na nyara za Serikali na uhujumu uchumi.

Alidai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kinyume na sheria ya uhifadhi wa wanyamapori na ile ya uhujumu uchumi Julai 28, mwaka huu, Kata ya Vikumburu, Tarafa ya Chole, wilayani Kisarawe.
Aliendelea kuwa walikutwa na meno 70 ya tembo yenye uzito wa kilo 306.5, bila kibali cha Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori. Baada ya kusomwa hati hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Bahati Ndeserua, alisema washtakiwa hawawezi kupata dhamana kwani mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza shauri hilo.
Hakimu Ndeserua aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14, itakapotajwa tena.

Awali, saa 6:30 mchana polisi wawili; D 8656 Koplo Senga Idd Nyembo (47) na G 553 PC Issa Mtama (29), walifikishwa mahakama ya kijeshi Polisi Makao Makuu Mkoa wa Pwani, kusomewa mashtaka ya kijeshi na kufukuzwa kazi.

Washtakiwa wengine ni Prosper Maleto (36) mkazi wa Tandika Kilimahewa, Seif Kadro (35) mkazi wa Panga la Mwingereza Chole, Ramadhan Athuman (45) mkazi wa Chanika, Mussa Ally (35) mkazi wa Kinondoni, Said Mdumuka (28) mkazi wa Panga la Mwingereza, Amir Bakar (33) na Hamad Salum (35) dereva wa gari lililokuwa likisafirisha meno hayo.

No comments:

Post a Comment