Pages

Sunday, August 18, 2013

Ponda azua hofu •Waislamu kukutana leo kutoa msimamo

 Habari na Tanzania Daima.
HOFU ya kutokea vurugu za kidini imeanza kuyakumba baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya sakata la kupigwa risasi Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda.

Juzi idadi kubwa ya askari polisi walikuwa wakirandaranda nje ya misikiti baada ya kuwapo taarifa za waumini wa Kiislamu kufanya maandamano ya kutaka ukweli wa sakata la kiongozi huyo uanikwe.

Hata hivyo maandamano hayo hayakufanyika na ikatangazwa kuwa leo katika viwanja vya Nurul Yakin wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam kutafanyika mkutano mkubwa.
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajabu Katimba, alisema wanapinga kupigwa risasi kiongozi wao, kusomewa mashtaka akiwa hospitalini na kupelekwa gerezani kabla hajapata ahueni.

Anasema katika mkutano huo watalizungumzia suala hilo kwa mapana na watapata msimamo wa pamoja juu ya kulishughulikia.
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Simba, juu ya mkutano huo ambapo alisema yeye si msemaji wa Shura ya Maimamu.

Alisema Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zipo kisheria, hivyo zina mipaka yake na zinafanya mambo kulingana na taratibu zilizojiwekea.
Alisema yeye ana mamlaka ya kuzungumzia masuala yanayohusu Baraza Kuu la 

Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Wakati sakata hilo likizidi kuwa tete, familia ya Sheikh Ponda imesema inakusanya ushahidi wa tukio la kupigwa risasi kwa kiongozi huyo na itauweka hadharani ukikamilika.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, msemaji wa familia ya Sheikh Ponda, Is-haq Rashid, alisema licha ya ndugu yake kuwa gerezani, familia inaendelea kukusanya ushahidi wa kilichotokea Morogoro na watakapokamilisha watauweka hadharani.
Alisema miongoni mwa ushahidi wanaoukusanya ni taarifa za daktari aliyemtibu Sheikh Ponda kwa mara ya kwanza mkoani Morogoro.

“Tumechoshwa na udhalilishaji aliofanyiwa ndugu yetu, sasa tumeamua kuweka hadharani ushahidi wa maovu yaliyofanywa na polisi,” alisema.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa sakata la Ponda hivi sasa linaipa wakati mgumu serikali na Jeshi la Polisi ambalo awali lilikanusha kumpiga risasi kiongozi huyo.
Inadaiwa serikali inahofia sakata hilo litakuza tofauti za kidini zilizoanza kujitokeza hivi sasa miongoni mwa jamii lakini pia kulipaka matope Jeshi la Polisi.

Inaelezwa kukamatwa kwa askari anayedaiwa kufyatua risasi katika msafara aliokuwemo Sheikh Ponda kunalenga kutuliza hali ya mambo iliyoonekana kuiendea vibaya serikali na vyombo vyake.

Tanzania Daima Jumapili limeelezwa licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, kukana jeshi hilo kuhusika katika tukio hilo, serikali imeamua kulivalia njuga ili kutuliza hasira za waumini wa kiongozi huyo wa kidini.

Kauli ya kamanda huyo ilizidisha hasira miongoni mwa wanaomuunga mkono Sheikh Ponda, huku wakitaka Shilogile ajiuzulu kwa kusema uongo. Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa tayari msako wa kumtafuta daktari aliyemtibu kwa mara ya kwanza kiongozi huyo wa kidini umeanza.

Daktari huyo inadaiwa ndiye aliyeweka wazi kuwa jeraha la Sheikh Ponda limetokana na risasi, ingawa hadi sasa hospitali na jina la daktari huyo havijawekwa wazi.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Kamanda Shilogile alisema wanafanya jitihada za kumjua daktari na hospitali aliyopatiwa matibabu kwa mara ya kwanza Sheikh Ponda.

“Polisi hatuna taarifa sahihi ya wapi alikotibiwa kiongozi huyo, tunafanya jitihada za kujua ni wapi alikotibiwa, habari kuwa alitibiwa hospitali fulani hapa Morogoro hazina ukweli,” alisema.

Tanzania Daima Jumapili lilitaka kujua kwanini polisi wanamshikilia askari anayedaiwa kufyatua risasi hewani katika harakati za kumkamata Sheikh Ponda wakati walisema hawahusiki.

Kamanda Shilogile alikataa kulitolea ufafanuzi jambo hilo kwa madai kuwa kuanzia sasa suala la Ponda litakuwa likizungumzwa na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi waliounda tume ya kulichunguza.

No comments:

Post a Comment