Pages

Tuesday, September 24, 2013

Adaiwa kutapeli akijifanya Ofisa Usalama wa Taifa.

MKAZI wa Mbagala, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Rashidi Mwinyimkuu, anadaiwa kutapeli watu fedha na vitu mbalimbali kwa kujifanya ni Ofisa Usalama wa Taifa.

Mwinyimkuu anayedaiwa kuwa karibu na baadhi ya askari amekuwa akifanya vitendo hivyo kwa muda mrefu sasa bila vyombo vya dola kumtia hatiani huku taarifa zake zikidaiwa kufikishwa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Charambe.

Wakizungumza kwa wakati tofauti na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, baadhi ya wakazi hao walisema watu kama hao wamekuwa wakichafua heshima ya serikali.

Walisema Mwinyimkuu alifanikiwa katika baadhi ya vitendo vyake vya utapeli kwa sababu alikuwa ana kitambulisho kilichokuwa kikimtambulisha kuwa ni Ofisa Usalama wa Taifa.

Katika tukio la hivi karibuni, Mwinyimkuu alimtapeli Ibrahimu Kipande sh 200,000, akidai kuwa angempatia kazi ya udereva kwenye moja ya Ofisi za Uslama wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Tulianza kumtilia shaka kutokana na tabia yake ya kupenda kujifaragua mbele za watu kwa kujitambulisha kila anapokutana na watu akisema mimi ni Ofisa Usalama hata bila kuulizwa,” alisema Kipande.

Hata hvyo baada ya kushindwa kutekeleza ahadi yake, Kipande alilifikisha suala hilo kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Charambe ambako mkuu wa kituo hicho alilimaliza kimya kimya, kwa mdai kulipwa fedha zake.

Kwa upande wake Mwinyimkuu, alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote.
“Sijafanya kazi ya Usalama wa Taifa na wala sijajifanya hivyo, mimi watu wote huku kwetu wananijua kazi yangu kuwa ni mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hadi kupachikwa jina la Mwinyimkuu CCM,” alisema Mwinyimkuu.

Mkuu wa Kituo hicho cha Polisi, Jonas, alisema anamfahamu mtu huyo kama mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Chalambe, lakini hajafikishwa kwenye kituo hicho kwa tuhuma hizo za utapeli.

No comments:

Post a Comment