Pages

Sunday, September 1, 2013

Lady Jaydee afunika uzinduzi ‘Foolish Age’.

MSANII Judith Wambura ‘Lady Jaydee,’ juzi usiku aliubeba uzinduzi wa filamu ya ‘Foolish Age,’ iliyochezwa na Elizabeth Michael Lulu uliofanyika Ijumaa usiku katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
 
Jaydee aliyepanda jukwaani baada ya tukio la uzinduzi wa filamu hiyo akikaribishwa na Lulu aliyetamka wazi kuwa amekuwa akimpenda Jaydee ‘Anakonda’ tangu utotoni mwake, aliufanya ukumbi urindime kwa mayowe ya shangwe na nderemo.
 
“Napenda kuwashukuru watu wote mliofika hapa Mlimani City katika uzinduzi wa filamu hii ambayo naamini italishika soko ipasavyo kwa sababu imechezwa kwa umahiri mkubwa,” alisema Lulu na kuamsha shangwe za aina yake.

Lulu hakuishia hapo, ndipo akasema atakuwa mchoyo kama asingemtaja Lady Jaydee aliyekuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliofika katika tukio hilo la historia maishani mwake.

“Lady Jaydee nakupenda sana, njoo dadangu, nilikuwa nakupenda sana tangu nilipokuwa mdogo hadi sasa bado nakupenda,” sauti ya Lulu ilisikika ukumbini kupitia kipaza sauti.
Kilichofuata ni Jaydee kwenda jukwaani na moja kwa moja akaanza kuimba wimbo wa 

‘Njiwa Peleka Salamu’ wa mkongwe Patricia Hillary aliyewainua mashabiki na kuwaambia wanaruhusiwa kucheza, watu wakaamua kuacha viti na kwenda kucheza mduara.

Kuanzia hapo, ikawa ni bandika-bandua kwani aliunganisha kibao chake cha Joto Hasira,’ hivyo kuibua shangwe, nderemo zilizoambatana na mbinja kiasi cha kuufanya ukumbi kuzizima kabla ya kuongeza kibao cha Yahya.

Wakati akiimba vibao hivyo, wapenzi na mashabiki walishindwa kutulia kwenye viti vyao na kwenda kumtunza noti zisizo na idadi hadi kulazimika kusimama kwa muda akusanye kwanza fedha zake kabla ya kuendelea kuwaburudisha mashabiki wake.
Wakati wa kibao cha ‘Yahya,’ Lulu akaibuka nyuma ya jukwaa na akaungana na Jaydee kuimba hali ambayo iliongeza mvuto hadi wapenzi na mashabiki kumtunza fedha binti huyo nyota wa filamu.
 
Baada ya wimbo huo, Lulu alisema amefurahi kuimba na Lady Jaydee kiasi cha kutamani siku moja aje kuwa mwanamuziki.
Uzinduzi huo wa filamu hiyo ya Lulu aliyocheza baada ya kutoka mahabusu alikokuwa akishikiliwa kwa miezi kadhaa kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Steven Kanumba, ulishuhudiwa na wasanii kadhaa kama Amini Mwinyimkuu, Barnaba wa THT na wale wa Bongo Movie.

No comments:

Post a Comment