Pages

Tuesday, September 10, 2013

Operesheni kamata daladala yakera abiria jijini Dar es Salaam.

KIKOSI cha Usalama Barabarani jijini Dar es Salaam kimelaumiwa kwa kuendesha operesheni ya kuzikamata daladala bila ya kufuata utaratibu na kusababisha usumbufu kwa abiria.

Wakizungumza kwa wakati tofauti jijini Dar es Salaam juzi, wakazi hao walisema hata kama walikuwa na lengo zuri la kukamata magari mabovu bado walipaswa kuwa wabunifu, kwa kutafuta utaratibu mwingine wa kupunguza uhaba wa usafiri.

Mmoja wa wakazi hao, Said Mohamed, alisema operesheni hiyo iliyoendeshwa mwishoni mwa wiki abiria katika barabara ya Morogoro ilisababisha abiria kukaa vituoni kwa muda mrefu kutokana na wamiliki wengi kuondoa magari yao barabarani ili kukwepa kukamatwa.

Hamisi Mohamed, dereva wa daladala, alisema amekuwa akishangazwa na askari hao, pindi wanapowakamata huwarundikia makosa, ili watoe rushwa kwa askari hao.

“Utaona askari huyo anakujia kwa vitisho, mara kachukua leseni au utamuona anang’oa kibao cha namba ya gari, lakini ukishampatia kile anachotaka analiachia gari,” alisema.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, aliwataka wananchi wawe watulivu wakati kikosi hicho kinapotekeleza sheria ya kuyakama magari mabovu barabarani.

Alitoa wito kwa wananchi kuwa watakapomuona askari aliyekamata gari bovu halafu katika mazingira yasiyoeleweka akaliachia, wampelekee taarifa ili askari huyo ashughulikiwe.

Aidha, alimtaka mwadishi kuwasiliana na Ofisa wa Kikosi hicho cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, Amir Konja, ili ampatie idadi ya magari mabovu yaliyokamatwa katika zoezi, ambalo limeendeshwa kwa mafanikio makubwa.

Hata hivyo, Konja alishindwa kutoa ushirikiano tena kama alivyofanya juzi wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi: “Siwezi kulizungumzia hilo, kwa bahati mbaya niko hospitali nina mgonjwa”.

No comments:

Post a Comment