Pages

Sunday, September 1, 2013

Ujambazi tena Dar...yamezidi kushika kasi siku ya jana tena.

MATUKIO ya ujambazi katika Jiji la Dar es Salaam yamezidi kushika kasi baada ya jana majira ya saa 3:00 asubuhi watu wawili waliokuwa katika pikipiki aina ya Boxer kumpora mwanamke mamilioni ya fedha kwa kutumia silaha.

Tukio hilo limetokea siku mbili baada ya matukio mawili ya aina hiyo kutokea katika jiji hilo mojawapo likitokea katika Benki ya Habib, iliyopo makutano ya Barabara ya Livingstone na Uhuru  na kufanikisha uporaji wa mamilioni ya shilingi za Kitanzania pamoja na dola za Marekani 181,885.

Jingine lilitokea maeneo ya Gymkhana, makutano ya Barabara ya Barack Obama na kuhusisha raia wawili wa Kenya ambao ni ndugu, Mark Rubila(16) na Sila Rubila(21) kutoka mji wa Kakamega ambao walimuua kikatili dereva teksi Ramadhani Mahembe(38), maarufu kama ‘Mjomba Mjomba’ au ‘Papaa’ mkazi wa Buguruni Chama.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio la jana, mwanamke huyo aliporwa fedha hizo katika kituo cha basi cha Kwa Aziz Ally, Wilaya ya Temeke, dakika chache baada ya kushuka ndani ya daladala akitokea Mbagala.

“Baada ya kushuka mwanamke huyo ambaye alikuwa na begi alisimama kituoni hapo akisubiri  usafiri mwingine lakini ghafla ilikuja pikipiki aina ya Boxer iliyokuwa na watu wawili na kumpora begi hilo lililokuwa na pesa ambazo kiasi chake bado hakijajulikana,” alisema shuhuda mmoja.

Kabla ya kupora, majambazi hayo walifyatua risasi ambayo ilimjeruhi mwanamke huyo na abiria mwingine aliyekuwa kituoni hapo akisubiri gari.

“Hili tukio ni la kupanga kwani haiwezekani mtu atokee sehemu akiwa na mzigo wake kisha afikie kuporwa hivi hivi, inaonekana kuna watu walijua kila kitu kuhusu mwanamke huyo na kumfuatilia na walijua fedha hizo anazipeleka wapi,” alisema shuhuda mwingine.
Katika hatua nyingine, watuhumiwa waliohusika katika tukio la mauaji ya dereva teksi Mahembe, walitoa siri kuwa walitaka kupora gari la dereva huyo ili wakaliuze.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine maeneo ya Kimara Bonyokwa wakiwemo raia wa Kenya, wakiwa na gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 230 ABV ambalo pia ni la wizi.
Watuhumiwa hao ni Ramadhani Rashidi(32) na Hamisi Rashidi(36).

No comments:

Post a Comment