Pages

Monday, September 23, 2013

Vodacom yawaomba radhi wateja wake..kukosekana kwa huduma ya M-Pesa kwa saa takribani nane nzima Septemba 21,2013.

KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom imesema kukosekana kwa huduma ya M-Pesa kwa saa takribani nane nzima Septemba 21 mwaka huu, kunatokana na kuzidi kwa muda uliokuwa umetengwa kwa ajili ya maboresho ya kawaida katika mfumo wa huduma hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Rene Meza, alisema jana kuwa kazi ya uboreshwaji wa mfumo wa huduma hiyo ilipangwa kufanyika kwa saa sita, lakini matatizo mengine ya kiufundi yalisababisha kufanyika zaidi ya muda uliopangwa.

“Tunapenda kuwaomba radhi wapendwa wateja wetu, washirika wetu na benki zote pamoja na wananchi wote kwa ujumla kwa kutoweza kutumia huduma yetu ya M-Pesa kutokana na kazi ya kuboreshwa kwa mtandao wa huduma hiyo.

“Kazi ya uboreshaji wa mtandao huo ilikwenda vizuri, lakini mabadiliko hayo yalisababisha kutokea kwa matatizo kadhaa ya kiufundi ambayo yalidumu kwa saa nane, hali iliyotulazimu kusitisha baadhi ya huduma za mtandao wa M-Pesa,” alisema Meza.
Aidha, alisema baada ya kugundua chanzo cha tatizo hilo, wataalamu wa kampuni hiyo waliendelea kufanya marekebisho hayo kwa umakini na kuweza kugundua chanzo cha tatizo na kurudisha huduma hiyo katika hali yake ya kawaida.

No comments:

Post a Comment