Pages

Monday, October 7, 2013

Serikali yapongeza Tamasha la Pasaka.

SERIKALI kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), imewapongeza waandaaji wa Tamasha la Pasaka, Kampuni ya Msama Promotions kutokana na ubora wake mwaka huu na kuwataka kuendeleza mipangilio hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa kupokea ripoti na kutathimini tamasha la mwaka huu lililofanyika kwenye mikoa mitano hapa nchini, Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa wa Basata, Nsao Shalua, alipongeza jitihada na mipango inayofanywa na Msama katika kuliendeleza tamasha hilo.

Shalua aliongeza kuwa michango inayotolewa na kampuni hiyo kwa jamii kupitia matamasha hayo ni mfano wa kuigwa na kuwasihi wadau wengine kushiriki na kuchangia katika kutunisha mfuko wa matamasha ya Pasaka.

Naye Ofisa Sanaa Mkuu, Philemon Mwasanga, alitoa wito kwa kampuni hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Alex Msama, mbali ya kujenga kituo cha kulea watu wenye uhitaji maalumu ambao ni wajane, walemavu na yatima kitakachokuwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wawe na mkakati maalumu wa kuvumbua na kuibua wasanii wachanga katika tasnia ya muziki wa injili hapa nchini, kwa sababu muziki wa sasa umemezwa na teknolojia.

Mwasanga aliwataka waandaaji hao kuazimia kuanzia mwakani, kuacha matumizi ya CD wawapo jukwaani ili kuuokoa muziki ambao unapoteza mwelekeo wake hasa kimataifa.

Aidha, Mwasanga alitumia fursa hiyo kumsihi Msama kununua vyombo vyake vya muziki ili kufanikisha matamasha yake ili waimbaji waonyeshe vipaji vyao katika tasnia ya muziki.

“Ili kuendana na kasi ya muziki katika hadhi ya kimataifa, unaweza kutakiwa nchi za wenzetu, ili ukidhi inatakiwa kujipanga kimataifa katika utayarishaji na sio matumizi ya (mshindo nyuma) CD,” alisema.

Mwasanga alisema mtindo huo umepitwa na wakati, waimbaji wanatakiwa wajizoeze kumiliki jukwaa kwa kuimba na kupiga moja kwa moja.

Kwa upande wake, Ofisa Matukio wa Basata, Kurwijira Maregesi, alisema matamasha yajayo yawe ni mfano wa kuigwa kinidhamu na muonekano wa mavazi kwa waimbaji.

Maregesi alisema waimbaji wanaume wajiepushe na uvaaji wa hereni masikioni, kusuka nywele na kuvaa suruali chini ya makalio, kwa kuwa muziki wa injili unamtukuza Mungu.

Ili kunogesha tamasha lijalo, Ofisa wa Basata, Vick Temu alipendekeza kuwepo kwa ‘Projector’ zitakazofungwa uwanjani ili kuwapunguzia bughudha watazamaji watakaoukuwa mbali na jukwaa kuu.

Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Abihudi Mang’era, ilitoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ambayo matamasha yalifanyika, licha ya fununu za matishio ya ugaidi zilizosambazwa.
Mang’era alisema tamasha lijalo litakuwa la kimataifa zaidi, kwa sababu litaongeza idadi ya mikoa na waimbaji wa kimataifa. Kwamba lina malengo ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuingia nchi za jirani.

No comments:

Post a Comment