Pages

Wednesday, October 30, 2013

VIJANA WAPINGA KODI YA SIMU

Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda.
BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeitaka Serikali kurejesha bungeni kwa hati ya dharura Muswada wa Marekebisho ya Tozo ya Sh 1,000 kwa laini za simu kwa mwezi.

UVCCM imesema ikiwa tozo hiyo itatekelezwa, itanyima Watanzania zaidi ya milioni nane haki ya msingi ya mawasiliano na huduma za kupokea na kutuma fedha kwa mtandao, jambo ambalo pamoja na kwamba lililenga kuongeza mapato, ni dhahiri litayashusha.
Sambamba na hilo, Baraza limempa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza siku 21 kutoa kwa umma hatua anazochukua ili kuokoa wakulima wa korosho nchini dhidi ya unyonyaji, unaofanywa na walanguzi wa zao hilo.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda aliwaambia waandishi wa habari jana katika ofisi za Makao Makuu ya CCM mjini hapa kuwa maazimio hayo yalifikiwa na Baraza Kuu la Umoja huo katika kikao chake cha siku moja jana, chini ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sadifa Juma Hamis.
Kwa mujibu wa Mapunda, katika kikao hicho walijadili migogoro ya wafugaji na hifadhi, taarifa ya utekelezaji wa tozo ya Sh 1,000 kwa laini za simu na masuala ya wakulima wa korosho.

Kuhusu tozo ya Sh 1,000, Mapunda alisema: “Baraza limejadili kwa kina na kubaini athari zinazoweza kutokea kutokana na tozo hiyo kwamba ni pamoja na ugumu wa ukusanyaji Sh bilioni 178 kwa mwezi katika bajeti ya mwaka 2013/14 ambao utaratibu wake unazorotesha na kurudisha nyuma juhudi za kisekta kuwezesha mawasiliano kwa wote.

“Lakini idadi kubwa ya wateja milioni nane ambao ni wa kipato cha chini watakosa huduma. Kushindwa kufikia watu wengi kwa huduma zaidi ya milioni nane kati ya idadi ya watumiaji milioni 26, ni dhahiri wakiondolewa kwenye mfumo wa mawasiliano, mapato yatashuka kwa watoa huduma na Serikali,” alisema Mapunda.

Kutokana hilo, alisema Baraza Kuu la UVCCM linaitaka Serikali kuzingatia mazungumzo ya Julai 23 ya Rais Jakaya Kikwete na watoa huduma za mawasiliano ya simu nchini baada ya Rais kukubali kuwapo ugumu wa utekelezaji wa hilo hasa namna ya ukusanyaji wa fedha na ukosefu wa mawasiliano kwa watu wenye kipato cha chini.

Kuhusu wakulima wa korosho, Mapunda alisema Baraza lilijadili changamoto za wakulima wa korosho nchini ikirejea uamuzi wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mei mjini hapa kuhusu matatizo ikiwamo kuyumba kwa bei ya korosho, malipo kuchelewa, tozo nyingi na udhaifu wa baadhi ya vyama vya ushirika.

“Baraza Kuu limeamua kwa pamoja kuwa hali hiyo haivumiliki na wananchi wana haki ya kulalamikia matatizo hayo, pia limesikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu ya CCM la Mei lililoitaka Serikali iwaite wadau wote na kuchukua hatua mapema,” alisema Mapunda.

Alisema kutokana na hilo, Baraza Kuu linamtaka Waziri Chiza kufanya uamuzi wa dharura wa kushughulikia matatizo hayo katika kipindi cha siku 21 na kutoa kwa umma hatua alizochukua na atakazoendelea kuchukua kuokoa wakulima wa korosho na unyonyaji hasa wa bei kuyumba.

Mapunda alisema Baraza Kuu lilijadili migogoro ya wafugaji na hifadhi, hasa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara inayopakana na hifadhi ya Serengeti na mkoa wa Lindi, ambako wilaya zake za Kilwa na Liwale zinapakana na Hifadhi ya Selous kuwa kumekuwa na unyanyasaji mkubwa.

Alisema wafugaji na askari wa wanyamapori na wa kampuni ya uwekezaji ya Gurumeti, wamekuwa wakinyanyaswa na kutozwa kiwango cha Sh 50,000 hadi Sh 300,000 kwa ng’ombe mmoja bila stakabadhi na walitaka watendaji wa Serikali wasikae kimya wakati wananchi wananyanyaswa.
CHANZO NI HABARI LEO

No comments:

Post a Comment