Pages

Monday, October 7, 2013

YANGA JANA WALIENDELEZA WIMBI LA USHINDI BAADA YA KUICHAPA MTIBWA SUGAR MABAO 2 - 0.

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga jana waliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani, Morogoro kwa mabao 2-0.
 ...dakika sita tu kuanza kucheza na nyavu kwa bao la Mrisho Ngasa
Kwa matokeo hayo, Yanga wamefikisha pointi 12 baada ya kushuka dimbani mara saba na kuchupa hadi nafasi ya pili nyuma ya watani zao Simba wenye pointi 15.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, 
 Yanga iliwachukua dakika sita tu kuanza kucheza na nyavu kwa bao la Mrisho Ngasa akimalizia pasi safi ya Mrundi Didier Kavumbagu.
Kama haitoshi, dakika ya 20, Kavumbagu naye alimsalimia kipa wa Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif kwa kupachika bao la pili akiitumia pasi ya Ngasa.

Mtibwa walijibu mapigo, lakini Vicent Barnabas alishindwa kuitendea haki pasi ya Ally Shomari dakika ya 23, wakati alipopiga nje mpira kwa kichwa, kabla ya dakika ya 33, Ngasa kubaki na Kipa Sharrif lakini shuti lake jepesi likadakwa.

Hadi mwamuzi Isihaka Shirikisho anapuliza filimbi kuashiria mapumziko matokeo yalikuwa 2-0.
Kipindi cha pili, Mtibwa ilizinduka hasa baada ya kufanya mabadiliko kadhaa, lakini bahati haikuwa yao.

Awali kabla ya kuanza kwa mchezo, Yanga walizuia Azam TV kurusha mechi yao hiyo ya nyumbani kwa madai kuwa mazungumzo bado yanaendelea.

Azam TV walirejesha kamera zao dakika ya 40 na kuendelea na kazi, baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuingilia.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema walilazimika kuingilia kati, kwani suala hilo ni la kimkataba, hivyo mechi kuonyeshwa ni mali ya shirikisho hilo na Azam TV, wala sio klabu.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Kelvin Yondani, Athumani Idd ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza/Said Bahanuzi.
Mtibwa: Hussein Sharrif, Hassan Ramadhani, Paulo Ngalema, Salvatory Ntebe/Dickson Daudi, Salim Abdallah, Shabani Nditi, Ally Shomari, Awadh Juma, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Shabani Kisiga, Vicent Barnabas/Masoud Mohamed.

No comments:

Post a Comment