Pages

Saturday, November 16, 2013

WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA, NDUGU WAANGUA VILIO!

Stori: Mbeya Yetu
NDUGU wa watuhumiwa wawili kati ya wanne waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana hatia la kumuua aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja waliangua vilio baada ya hukumu hiyo.
 
Marehemu  John Mwankenja, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe enzi za uhai wake.
Jumatano iliyopita, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya aliyekuwa ikiendesha vikao vya kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Samuel Karua alipotoa hukumu hiyo, baadhi ya ndugu wa waliohukumiwa walilipuka kwa vilio kutokana na uchungu wa adhabu hiyo.
      Kushoto hakimu Mwakalinga ambaye ni mshtakiwa wa kwanza kuhukumiwa kunyongwa.
Hukumu ya kesi hiyo iliahirishwa kutolewa zaidi ya mara tatu na kuzua hali ya sintofahamu kwa ndugu wa washtakiwa na wafuatiliaji wa kesi hiyo, wengi wakihoji kulikoni!

Kabla ya kusoma kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Archiles Mulisa aliwataja watuhumiwa wote wanne kuwa ni Hakimu Mwakalinga, Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili na Kelvin Myovela wanaokabiliwa na tuhuma za kumuua kwa makusudi John Mwankenja.
Baadhi ya wananchi wakiwa nje ya mahakama.
Alisema watuhumiwa hao wenye kesi namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika Kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Karua ambaye alianza majira ya saa 8:37 mchana na kumaliza saa 9:37 alasiri alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka na utetezi haubishani kuhusu kifo cha marehemu.
Aliongeza kuwa pande hizo pia hazibishani kuhusu ripoti za kitaalam na dhamira za mauaji hayo bali kinachobishaniwa ni uhusika wa watuhumiwa hao dhidi ya mauaji hayo.
Alisema katika kutetea hoja zao upande wa mashtaka ulipeleka mahakamani mashahidi 11  wakiongozwa na shahidi namba moja aliyewatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.
Shahidi huyo namba moja Weston Jacob (17) mkazi wa Kiwira na mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kipoke ambaye pia ni mjomba wa marehemu ambaye aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio akiwa nyumbani saa 2: 30 usiku marehemu alifika na kupiga honi ya gari akitaka afunguliwe mlango.
Kutokana na ushahidi huo, Jaji Karua alisema  mshtakiwa namba moja na namba mbili ambao ni Hakimu Mwakalinga na Daudi Mwasipasa wanatiwa hatiani kuhusika moja kwa moja na mauaji kutokana na kukiri kwao kwa mlinzi wa amani, mchukua maelezo na  vipimo vya vinasaba.
Alisema mshtakiwa namba tatu, Obote Mwanyingili yeye anatiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji hivyo yeye hausiki na kosa hilo.
Jaji Karua alisema mshtakiwa namba nne, Kelvin Myovela anatiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika katika mauaji hayo ingawa hakuhusika na kitendo hicho.
Kutokana na ushahidi huo, Jaji Karua alisema washtakiwa namba moja na namba mbili wanahukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Aliongeza kuwa, mshtakiwa namba tatu aliyemhifadhi mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka saba, mshtakiwa namba nne,  Kelvin Myovela aliyehifadhi silaha iliyotumika kwenye mauaji hayo atatumikia kifungo cha  miaka saba.

No comments:

Post a Comment